Tume Huru ya Uchaguzi nchini Nigeria – INEC, imesema zoezi la kuhesabu kura linarndelea licha ya kasoro kadhaa ikiwemo vibanda kadhaa vya kupigia kura kuharibiwa na kuporwa, na mashine za kusoma vitambulisho kuibwa katika baadhi ya majimbo.
INEC imesema, karibu watu milioni 90 wamepiga kura katika uchaguzi huo ambao kwa sehemu kubwa ulikuwa wa amani, licha ya visa vya hitilafu za kawaida xa kiufundi kuchangia na ucheleweshaji zoezi la upigaji kura hadi saa za usiku wa jana, Februari 25, 2023.
Uchaguzi huo umefanyika huku kukiwa na ushindani wa kihistoria kati ya wagombea watatu wanaowania Urais wa Taifa hilo linaloongoza kwa idadi ya watu barani Afrika, ili kumrithi Kiongozi anayemaliza muda wake, Mohamud Buhari.
Aidha, tume hiyo imesema leo Jumapili Februari 26, unafanyika uchaguzi katika vituo 141 kwenye jimbo la Bayelsa la kusini mwa Nigeria, baada ya zoezi hilo kusimama kufuatia kujitokeza kwa vurugu na mivutano ya kisiasa na sasa limefanyika kwa amani na utulivu.
Katika nafasi ya urais, mvutano upo baina ya Meya wa zamani wa Lagos, Bola Tinubu (70), anayegombea kwa tiketi ya chama cha APC, na Atiku Abubakar (76) wa PDP, anayewania kwa mara ya sita kutaka wadhifa huo mkubwa Kitaifa.
Hata hivyo, kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999, mgombea wa tatu, Peter Obi wa chama cha Labour anaonekana kuupa changamoto udhibiti wa vyama hivyo viwili, akiendesha kampeni zake chini ya kauli mbiu ya mageuzi huku akipigiwa upatu kushinda Urais wa Nigeria.