Serikali nchini, imesema vifo vya watu wawili vilivyotokea kwa ulaji wa nyama kwenye kijiji cha Msaranga kilichoko Kata ya Kisale, Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro Mei 4, 2023 havina uhusiano na ugonjwa wa kimeta.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mifugo Tanzania, Dkt. Benezeth Lutege imeeleza kuwa, wizara inawatoa wananchi hofu iliyojitokeza Wilayani Rombo, baada ya majibu ya uchunguzi wa kimaabara kuthibitisha kuwa vifo hivyo havihusiani kabisa na ugonjwa wa kimeta ambao hutokana na kula nyama ya ng’ombe aliyeathirika na ugonjwa huo.
Imesema, Wizara inawasisitiza wananchi wa Kijiji cha Msalanga, Kata ya Kisale Wilaya ya Rombo na watanzania wote kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari za kiafya ikiwa ni pamoja na kununua nyama zilizokaguliwa na wataalamu wa mifugo waliosajiliwa na Baraza la Veterinari Tanzania (VCT) na kutoka kwenye mabucha na maduka ya nyama yaliyothibitishwa na serikali kupitia Bodi ya Nyama Tanzania (TMB).
Aidha, taarifa hiyo pia imefafanua kuwa ni vyema wananchi wakajua dalili za ugonjwa wa kimeta ambazo ni pamoja na kifo cha ghafla kwa mnyama aliyeathirika za sehemu zote zilizo wazi hutoa damu ambayo haigandi.
Dalili zingine ni watu ambao hugusana au kula nyama ya mnyama mwenye kimeta, huonesha dalili za homa, kupumua kwa shida, kichefuchefu, kutapika na malengelenge kwenye ngozi dalili ambazo kwa mujibu wa taarifa hazikuonekana kwa wale wagonjwa wawili waliofariki katika tukio hilo na kwamba ni nadra sana kwa mnyama mwenye kimeta kupatiwa matibabu.