Naibu Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), David Silinde amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kujenga shule za wasichana katika mikoa yote 26 na ile iliyopo katika Halmashauri ya Namtumbo ikiwa ni miongoni wa shule 10 za kwanza nchini ambazo zimepatiwa fedha kwa mwaka huu.
Silinde ameyasema hayo hii leo Oktoba 18, 2022 wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Mkoani Ruvuma, alipokuwa akiongea na Wananchi wa Kijiji cha cha Migelegele mara baada ya kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Amesema, “Shule hizi zimetengewa shilingi bilioni 4 kila moja na zikikamilika zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 1,000 na 1,200 ambao watakuwa wanasoma masomo ya sayansi na bila shaka zitamkomboa mtoto wa kike kielimu”
Awali, Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa alisema anamshukuru Rais Samia kwa kutoa shilingi 15.5 bilioni kwa ajili ya shughuli za maendeleo wilayani humo huku akiishukuru Serikali kwa kuwapatia mradi ya maji wa shilingi 5 bilioni, ambao umesaidia wananchi kupata maji bila mgao.