Mawaziri wa Fedha na Mawaziri wa Jinsia Barani Afrika, wametakiwa kuhakikisha suala la kupambana na ukatili wa kijinsia linawekwa kwenye Sera, Mipango na Bajeti za nchi, ili litekelezwe kikamilifu huku Serikali ya Tanzania ikianza kushirikiana na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhakikisha masuala ya jinsia yanajumuishwa katika mipango na bajeti.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito huo jijini Dar Es Salaam wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa Mawaziri hao na kusema uwekaji wa suala la ukatili wa kijinsia kwenye Sera, mipango na bajeti itasaidia kufikia usawa wa kijinsia kwa vitendo.

Amesema, masuala mengine ni kuwawezesha wanawake kiuchumi ili kuweka usawa na haki katika umiliki wa rasilimali, ubunifu na teknolojia, ushiriki wa wanawake katika masuala ya Amani na usalama ikiwemo kupata elimu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi pamoja na suala la Afya kwa wanawake.

Aidha, Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania imeshaanza kushirikiana na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhakikisha masuala ya jinsia yanajumuishwa katika mipango na bajeti na kukaguliwa.

Awali, Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF AfRITAC East) Dkt. Xiangming Li, amesema washiriki wamehamasika na jinsi Tanzania inavyotekeleza suala la ushirikishwaji wa Wanawake.

10 wafariki kwa Mvua, tahadhari yazidi kutolewa
Washauriwa kuwajenga Watoto kiimani kuepuka uhalifu