Kanuni mpya za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania – TCRA, za mwaka 2023 na kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za 2023 (Usajili wa laini za simu), sasa zimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuwawezesha watanzania wengi kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi, ili kupata urithi wa kidijitali wa marehemu wao.
Hayo yamesemwa, na Kaimu Mkuu wa mawasiliano na uhusiano kwa umma wa TCRA, Rolf Kibaja na kuongeza kuwa Kanuni hizo ziliundwa kwa kuzingatia umuhimu wa urithi wa kidijitali, wa watumiaji wa simu za mkononi na haja ya kulinda taarifa zao muhimu.
Amesema ili kanuni hizo zifanye kazi na wahusika wanufaike ni lazima wawakilishi walioidhinishwa na wanafamilia kufuata taratibu za kisheria ili kuhifadhi urithi wa kidijitali wa watu waliofariki, na kuongeza kuwa mtumiaji wa simu ya mkononi anapofariki dunia, namba yake ya simu hurudishwa kwa kampuni husika ya mtandao wa simu.
“Namba hiyo inaweza tu kupangiwa mtu mwingine iwapo msimamizi wa mirathi atashindwa kuwasilisha nyaraka muhimu zinazomtambulisha kuwa mwakilishi aliyeidhinishwa wa mirathi ya marehemu,” amesema.
“Ni muhimu kutambua kwamba laini ya simu iliyohamishwa inabaki na taarifa zinazohusiana na mmiliki halisi, hii inajumuisha kumbukumbu za kifedha, data binafsi zilizosajiliwa kwa njia ya kibayometriki.”
“Hata ushahidi wa uhalifu ikiwa mtumiaji aliyefariki alihusika katika vitendo hivyo unaweza kupatikana, kwa hiyo lengo la uhamisho liko kwenye matumizi ya laini ya simu, wakati umiliki na faragha ya taarifa ya mtumiaji wa awali huhifadhiwa vizuri,” amesema.
Alisema, kanuni hizo pia zinashughulikia mchakato wa kubadilisha jina la mtumiaji ikiwa jina la mteja limesajiliwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Kitaifa (Nida), mabadiliko yoyote ya jina lazima yaripotiwe ili kuhakikisha uhifadhi sahihi wa kumbukumbu,” amesema.