Mamlaka za Usalama nchini Urusi, zimejitangazia ushindi wa umiliki wa eneo zima la Bakhmut, japo maafisa wa Ukraine wamesema kwamba mapigano bado yalikuwa yanaendelea katika mji huo ambao umeharibiwa vibaya.
Madai ya Ushindi yametolewa na wizara ya ulinzi ya Russia, pamoja na kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner, na kufuatiwa na ujumbe wa pongezi kutoka kwa rais wa Russia Vladimir Putin huku Makamanda wa Ukraine wakifutilia mbali taarifa hizo wakisema kwamba maapigano bado yanaendelea katika mji huo wa Bakhmut.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, akizungumza nchini Japan ameonekana kama anathibitisha kwamba ameupoteza mji wa Bakhmut, lakini maafisa wake wa mawasiliano wamesema kwamba matamshi yake yametafsiriwaa visivyo na kwamba alikuwa anajibu tu swali iwapo Russia inaudhibiti mji huo.
Madai ya Urusi yamejiri wakati wanajeshi wa Ukraine wanaripotiwa kupiga hatua muhimu katika wilaya za kaskazini na kusini mwa Bakhmut ambazo zimekuwa zikidhibitiwa na wanajeshi wa Russia kwa muda wa miezi 10, mamluki wa Wagner wakiwa wanaongoza mashambulizi.