Septemba 8, 2022, vyombo vingi vya Habari ikiwemo Dar 24 viliripoti kifo cha mtawala wa dola ya Uingereza Malkia Elizabeth wa Pili akiwa kwenye kasri lake la Balmoral huko Glosgow, nchini Uskochi.
Malkia Elizabeth anatajwa kutawala kwa muda mrefu wa miaka 70 katika historia ya utawala wa dola, amefariki akiwa na umri wa miaka 96.
Kifo chake kimeitingisha dunia nzima na Uingereza huwa imeweka taratibu rasmi zitavyokuwa baada ya kifo chake na nani atachukua madaraka yake ambapo tayari mtoto wake mkubwa wa kiume Mfalme Charles wa Tatu amekabidhiwa kiti hicho.
Ili kusoma nyakati za utaratibu wa kifo chake, basi unaanzia pale ambapo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kabla ya kutangazwa kwa kifo chake vipindi vya kawaida vilisitishwa na Watangazaji kuvaasuti na tai nyeusi.
Baada ya kifo chake, ujumbe wa ‘London Bridge Is Down’ ulitumwa na katibu binafsi wa Malkia kwa Waziri Mkuu Liz Truss ambapo Waziri Mkuu aliziarifu nchi 15 ulimwenguni, ambazo ni himaya ya Uingereza kupitia ujumbe maalumu.
Baadaye, akaziarifu nchi 36 zinazounda Jumuiya ya Madola (ikiwemo Tanzania), na viongozi wengine ulimwenguni. Hili hufanywa kabla ya umma kuarifiwa.
Bendera ya Uingereza na himaya zake ikashushwa na kupepea nusu mlingoni huku wavuti maalumu ya Kasri la Malkia ikibadilika rangi kuwa nyeusi, vivyo hivyo kwa kituo cha habari cha BBC ambacho kwa kawaida rangi zake ni nyekundu kikabadilisha na kuwa na rangi nyeusi.
Hata hivyo, kutakuwa na siku 10 za shughuli kadhaa kabla ya mazishi ya Malkia Elizabeth II na tayari Waziri Mkuu Liz Truss ambaye amekutana na Malkia mapema wiki hii, pamoja na mawaziri wake wataliona jeneza la Malkia likiwa St. Pancras, huku mrithi wa kiti cha ufalme Charles, akitaraji kuzuri miji mikuu ya nchi zinazounda Muungano wa Ufalme wa Uingereza ikiwemo ya Nothern Ireland, Scotland na Wales kabla ya maziko ya mama yake.
Kitakachojiri ndani ya siku kumi ni Charles kutangazwa kuwa Mfalme na ndipo mnyororo wa urithi wa kiti cha ufalme utabadilika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 70 na Shughuli za bunge nchini Uingereza pia zitasimama kwa siku 10.
Katika siku ya pili Waziri Mkuu ataliona jeneza la Malkia na kwa kuwa amefia Uskochi, sheria ya ‘Operation Union’ itapitishwa ili kuruhusu mwili wake kusafirishwa kwenda London, kwa treni ya kifalme endapo itafanyika kwa mujibu wa taratibu za kawaida na kama haitoamriwa kusafirishwa kwa treni, sheria ya ‘Operation Overstudy’ itapitishwa kuruhusu mwili wake kusafirishwa kwa ndege.
Aidha, katika siku ya nne, Mfalme Charles ataanza ziara kutembelea Muungano wa Ufalme wa Uingereza na mazoezi ya kubeba jeneza la Malkia kutoka Kasri la Buckingham kwenda Ukumbi wa Westminster yataendelea.
Katika siku ya tano, Jeneza litabebwa kutoka Buckingham hadi Westminster ambako misa itafanyika na hivyo kufanya taratibu za maziko kukamilika ambapo siku ya sita hadi siku ya mazishi mwili wa Malkia utabakia Kasri la Westminster kwa siku tatu ambapo umma utapata nafasi ya kutembelea na kutoa heshima za mwisho.
Hata hivyo, katika siku hiyohiyo ya sita, mazoezi ya mazishi yatafanyika na Viongozi wengine na watu mashuhuri kutoka kote ulimwenguni watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.
Kutokana na mwongozo wa msiba wake, siku ya mazishi itakuwa siku ya mapumziko Kitaifa na endapo itaangukia siku nyingine ya mapumziko ama wikendi, hakuna siku nyingine ya ziada itakayoongezwa ili kufidia.
Maziko ya Malkia Elizabeth yanatarajia kufanyika Westminster Abbey, na ibada ya mwisho itafanyika Kanisa la Mtakatifu George kwenye kasri la Windsor Castle, kisha Malkia atazikwa kwenye kanisa la Kumbukumbu ya Mfalme George wa Sita.
Kifo cha Malkia Elizabeth II kinatabiriwa kubadili siyo tu siasa za Uingereza, bali sehemu kubwa ya ulimwengu na wakati huu ambapo Malkia amefariki dunia, kiti cha enzi kinapitishwa mara moja bila sherehe yoyote kwa mrithi, Charles, Mkuu wa zamani wa Wales lakini zipo hatua kadhaa za kiutendaji – na za kitamaduni ambazo lazima azipitie ili kutawazwa kuwa Mfalme.
Moja kati ya vitu vya kwanza atakavyofanya ni kuamua kama atatawala kama Mfalme Charles III, au kuchukua jina lingine abapo ana uamuzi wa kutaka kutumia mojawapo ya majina ikiwemo la babu yake George VI aliyekuwa akiitwa Albert, ambaye alitawala kwa kutumia mojawapo ya majina yake ya kati.
Charles anaweza kuchagua kutoka kwa mojawapo ya majina yake manne – Charles, Philip, Arthur au George na ikumbukwe si yeye pekee ambaye amewahi kutakiwa kubadilisha jina lake na licha ya yeye kuwa mrithi wa kiti cha enzi, Prince William hatakuwa Mkuu wa Wales moja kwa moja ila itamlazimu pia kurithi jina lingine la baba yake, Duke of Cornwall.
Kufuatia mabadiliko hayo, Mkewe Catherine sasa atajulikana kama Duchess of Cornwall na kutakuwa na jina jipya pia la mke wa Charles, ya Malkia Consort – jina mbalo hutumiwa na mwenzi wa mfalme.
Hata hivyo, katika muda wa saa 24 au zaidi baada ya kifo cha mamake, Charles atatangazwa rasmi kuwa Mfalme na hii hii itafanyika katika kasri la St James’s huko London, mbele ya baraza la sherehe linalojulikana kama Baraza la kukabidhi Mamlaka linaloundwa na wajumbe wa Baraza la Siri, kikundi cha Wabunge wakuu wa zamani na wa sasa, na wenzao, baadhi ya watumishi waandamizi wa serikali, makamishna wakuu wa Jumuiya ya Madola, na Meya wa London.
Inaarifiwa kuwa, zaidi ya watu 700 wana haki ya kuhudhuria, lakini kutokana na ilani hiyo fupi, huenda idadi halisi ikawa ndogo kwani katika Baraza la kukabidhi Mamlaka mapema mwaka 1952, ni watu 200 pekee waliohudhuria hafla ya kutangazwa kwa mfalme ingawa utamaduni wa Taifa hilo hautamruhusu Mfalme kuwepo.
Aidha, katika mkutano huo, kifo cha Malkia Elizabeth kitatangazwa na Rais wa Baraza la Siri (anahisiwa kuwa ni Mbunge Penny Mordaunt ), na tangazo hilo litasomwa kwa sauti lakini maneno ya tangazo hilo yanaweza kubadilika, kwa utaratibu wa kitamaduni pia kutakuwa na sala, ahadi, kumpongeza mfalme aliyetangulia na kuahidi kumuunga mkono mfalme mpya.
Tangazo hili kisha linatiwa saini na watu kadhaa wakuu akiwemo waziri mkuu, Askofu Mkuu wa Canterbury, na Kansela na kama ilivyo kwa sherehe hizi zote, tahadhari ni kwamba yanaweza kuwepo mabadiliko ya kuongezwa au kusasishwa, kama ishara ya enzi mpya.
Baraza la kukabidhi Mamlaka litakutana tena na kwa kawaida siku moja baadaye na safari hii Mfalme atahudhuria akiwa na Baraza la Siri na hakutakuwa na uapisho kama ilivyo kwa mwanzoni mwa utawala wa mfalme wa Uingereza, kwa mtindo wa wakuu wengine wa nchi, kama vile Rais wa Marekani nk.
Hata hivyo, kutakuwa na tamko lililotolewa na Mfalme mpya kutokana na mila ya mwanzoni mwa Karne ya 18 yeye atakula kiapo cha kuhifadhi Kanisa la Scotland na baada ya shamrashamra za wapiga tarumbeta, tangazo la Charles kuwa Mfalme mpya litatolewa na kwenye roshani juu ya Mahakama ya Friary katika eneo la Kifalme la St James, na afisa anayejulikana kama Garter King of Arms.
Garter King of Arms atasema ”Mungu mwokoe Mfalme” na kwa mara ya kwanza tangu 1952, wimbo wa taifa utakapopigwa maneno yatakayosemwa ni ”Mungu Mwokoe Mfalme” kisha Risasi zitapigwa katika eneo la Hyde Park, ulipo Mnara wa London na upande wa meli za wanajeshi wa majini nao watafanya hivyo, kisha tangazo la kumtangaza Charles kama Mfalme litasomwa Edinburgh, Cardiff na Belfast.
Historia inaonesha kuwa, ishara ya juu ya kukabidhi mamlaka itakuwa ni kutawazwa, ambapo sasa Charles atavikwa taji rasmi na kutokana na maandalizi yanayohitajika, kutawazwa hakuwezi kutokea mara tu baada ya Charles kukabidhiwa madaraka maana Malkia Elizabeth alirithi kiti cha enzi Februari 1952, lakini hakutawazwa hadi Juni 1953.
Kwa miaka 900 iliyopita, kutawazwa kumefanyika kwa William the Conqueror aliyekuwa mfalme wa kwanza kutawazwa huko Westminster Abbey, na sasa Charles atakuwa wa 40 na huduma ya kidini ya Kanisa la Kianglikana, itafanywa na Askofu Mkuu wa Canterbury.
Katika kilele cha sherehe hiyo, ataweka Taji la la dhahabu la St. Edward juu ya kichwa cha Charles lililoanzia mwaka 1661 kikiwa ndicho kitovu cha Vito vya Taji kwenye Mnara wa London, na kwa sasa huvaliwa na mfalme pekee wakati wa kutawazwa kwenyewe (kutokana na kuwa na uzito wa 2.23kg).
Hatimaye, Mfalme mpya atakula kiapo cha kutawazwa mbele ya ulimwengu huku watu wakiwa wanatazama wakati sherehe hiyo ikiendelea na atapokea taji la umbo la duara na fimbo kama ishara ya jukumu lake jipya atakalopewa na Askofu Mkuu wa Canterbury ambaye ataweka taji imara la dhahabu juu ya kichwa chake.
Charles sasa atakuwa mkuu wa Jumuiya ya Madola, yenye nchi huru 56 na watu bilioni 2.4 kwa nchi 14 kati ya hizo ikiwemo Uingereza na zikijulikana kwa jina la Jumuiya ya Madola ambazo nyingine ni Australia, Antigua Barbuda, Bahamas, Belize, Canada, Grenada, Jamaica, Papua New Guinea, St Christopher na Nevis, St Lucia, St Vincent Grenadines, New Zealand, Solomon Visiwa Tuvalu.