Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi ametoa wiki mbili kwa wakazi wa jimbo la Ruangwa kuhakikisha kuwa wanajenga vyoo ili kujiepusha na ugonjwa wa kipindupindu.

Zambi amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Joseph Mkirikiti kufanya msako wa nyumba kwa nyumba ifikapo Januari 15, 2017 na endapo atakuta kuna mkazi wa kijiji chochote hajajenga choo, basi atozwe faisi ya sh. 50,000 mara moja.

Amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi na Chibula wilayani humo ambako alikuwa akiwasalimia wananchi kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu azungumze na wakazi wa vijiji hivyo.

Zambi amesema kuwa wakulima wengi wamevuna korosho msimu na baadhi yao wamelipwa vizuri, hivyo hawana budi kutumia sehemu ya fedha hizo kujenga vyoo ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko na hasa kipindupindu.

“Hili ni agizo la Serikali siyo yangu binafsi kwa hiyo ni amri halali. Kikilipuka kipindupindu, naanza na Mkuu wa Wilaya kabla na mimi sijaulizwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu au Mheshimiwa Rais,” amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka na ameamua kutumia muda huo kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo.

Mwalimu atiwa mbaroni baada ya kuishi kinyumba na mwanafunzi wake.
Jeshi la zimamoto kigamboni latoa mafunzo kwa taasisi mbalimbali