Serikali nchini, imeendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya kilimo ili kuinua Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja ikiwemo kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jijini Dodoma nakuongeza kuwa, hatua hizo ni pamoja na kuwezesha wakulima kupata mbegu bora zinazoendana na hali ya hewa nchini, kutoa ruzuku ya pembejeo hususan mbolea na mbegu na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia mpya na zana za kisasa.
Amesema, vipaumbele vingine ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani, kuongeza eneo la umwagiliaji kwa kuanzisha skimu mpya na kukarabati skimu za umwagiliaji zilizopo na upatikanaji wa masoko ya mazao ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha wakulima wananufaika na mauzo ya mazao.
“Katika mwaka 2022/2023, Serikali imesaini mikataba 31 yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 284.14 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji. Mikataba hiyo inahusu ujenzi wa mabwawa nane, skimu mpya 13 na ukarabati wa skimu za umwagiliaji 17,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, amesema ujenzi na ukarabati wa skimu hizo utaongeza eneo la umwagiliaji kwa hekta 50,930 na hivyo kufanya eneo la umwagiliaji kufikia hekta 778,210.6 kutoka hekta 727,280 mwaka 2021/2022.