Serikali nchini Afrika Kusini, imesema ipo tayari kuandaa mazungumzo kati ya Russia na Ukraine, huku Rais wa Russia, Vladimir Putin akipongeza pendekezo la amani la viongozi wa Afrika wanaotaka kumaliza mzozo kati ya nchi hizo mbili.
Waziri katika ofisi ya Rais wa Afrika Kusini Khumbudzo Ntshavheni ameyasema hayo na kuongeza kuwa, Kiongozi huyo alizungumza kwa simu na Putin, na kuelezea nia hiyo huku akisisitiza kuwa wapo tayari kuanda mkutano wa amani.
Amesema, “lazima tukubaliane na uwezekano wa Afrika Kusini kuandaa mkutano wa amani ambao utafanyika hapa, ukiwa sehemu ya mpango wa amani, na mahali utakapofanyika mkutano wa kilele huwa pamatafutwa, mahali pa kwanza unapoangalia ni uani kwako.”
Hata hivyo, Kiongozi huyo wa Russia “aliukaribisha mpango wa wakuu wa nchi za Afrika na kueleza nia yake ya kupokea ujumbe huo wa amani.
Mapema mwezi Mei, 2023 Rais Cyril Ramaphosa alisema Rais wa Urusi, Vladmir Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wote walikubali kuipokea timu ya amani yenye wajumbe sita kutoka barani Afrika.