Wataalamu kutoka Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma nchini Botswana, wameipongeza Tanzania kwa kuwa na mifumo imara ya ununuzi na utatuaji wa migogoro ya ununuzi na upataji wa wazabuni na wakandarasi wenye sifa za kutekeleza miradi ya maendeleo.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Msajili wa Mamlaka ya Zabuni ya Ununuzi wa Umma nchini Botswana, Geoffrey Gotshega, ambaye aliongoza ujumbe wake na kufanya ziara ya mafunzo Wizara ya Fedha na Mipango, ili kujifunza mambo mbalimbali kuhusu utekelezaji wa sera za ununuzi.
Amesema, “mifumo ya ununuzi ya Tanzania ni madhubuti kwa kuwa kanuni zake ni imara, ununuzi unafanyika kwa uwazi kwa njia ya kielektroniki na malalamiko yanafanyiwa kazi kwa uharaka na kuwezesha miradi kufanyika kwa wakati na kuipunguzia serikali gharama.”
Awali, Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma -PPAA, James Sando, alisema lengo la wataalam hao wa sekta ya uzabuni kuja Tanzania, ni kutaka kujifunza na kuangalia jinsi ambavyo Tanzania inafanya kazi ya ununuzi, na namna itakavyowasaidia katika utendaji kazi wao kwa sababu wamepitisha sheria yao ya ununuzi hivi karibuni.
“Tanzania tumeanza kutekeleza Sheria ya ununuzi miaka 23 iliyopita na tumekuwa na Mamlaka ya Rufaa, ndio maana wenzetu wamekuja kuangalia namna tunavyoendesha mashauri katika Mamlaka na wamefurahia ujuzi tuliowapa, pamoja na utekelezaji wa majukumu yao PPAA pia wanashughulikia mashauri ambayo yanatokea katika ununuzi wa umma nchini,” akisema Sando.
Mifumo imara ya ununuzi na utatuaji wa migogoro ya ununuzi nchini, imekuwa ikichangia kupata wazabuni na wakandarasi wenye sifa za kutekeleza miradi ya maendeleo na ujumbe huo kutoka Botswana, unaendelea na ziara hiyo ya mafunzo ambapo wajumbe hao wametembelea Wizara ya Fedha na Mipango na Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma -PPAA, jijini Dodoma.