Matukio ya maafa, yanayotokea na kusababisha madhara katika ngazi ya jamii ya atakiwa kushughulikiwa kuanzia Serikali ya Mtaa hadi ngazi ya Wilaya, kwa Viongozi na wataalamu kushirikiana na wadau pamoja na Wananchi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga hii leo Novemba 21, 2023 Mkoani Lindi wakati akifungua semina ya Masuala ya Maafa kwa Kamati ya Maafa Ngazi ya Mkoa na kuwasisistiza viongozi kuzingatia wajibu wao na kuwajibika ipasavyo kila mmoja katika eneo lake ili kuokoa maisha na kulinda mali za wananchi.
Amesema, “tumekutana leo kukumbushana wajibu muhimu mulionao kila mmoja kuwajibika katika eneo lake ili kuokoa maisha na kulinda mali za wananchi, tukumbuke Mkoa unaingia kusaidia juhudi za Halmashauri husika pamoja na kushirikisha uratibu wa msaada kutoka ngazi ya Taifa endapo madhara yatakuwa yamezidi uwezo wa rasilimali katika eneo husika.”
Ummy ameongeza kuwa “nisisitize Taasisi na Idara zinazohusika kuwa mstari wa mbele wakati wa tukio la maafa zinapaswa kujiandaa kikamilifu kwa kuweka utibu wa pamoja na kuwa na mpango wa dharula wa utendaji na utaratibu wa mawasiliano wakati wa dharula ili kuwezesha kuchukua hatua kwa haraka na kwa ufanisi ili kuokoa maisha.”