Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ametoka nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kudai kutoridhidhishwa na majibu ya Serikali kuhusu malipo ya fidia katika maeneo ya Mgodi wa Barrick North Mara Komarera, Nyamichele na Murwambe.
Waitara amefanya tukio hilo hii leo Mei 9, 2023 Bungeni jijini Dodoma, wakati wa kipindi cha maswali na majibu ambapo pia alikuwa akivua tai na koti lake wakati akitoka nje ya Bunge na kusema wanatarime leo wamemjua mbaya wao.
Katika swali lake, Waitara alihoji ni lini Wananchi hao watalipwa na alijibiwa kuwa “Mgodi wa Barrick North Mara ulionesha nia ya kutaka kuchukua baadhi ya maeneo ya Vijiji vya Komarera, Nyamichele na Murwambie ambavyo ni sehemu ya Vijiji vinavyozunguka mgodi huo.”
Aidha Serikali iliendelea kumjibu kuwa, “Baada ya Wananchi wa Vijiji hivyo kupata taarifa ya maeneo yao kuhitajiwa na mgodi wa Barrick North Mara, walianza kuongeza majengo harakaharaka (maarufu kama Tegesha), hali hiyo ilipelekea mgodi huo kuachana na maeneo hayo kwani hayaathiri uendeshaji wa shughuli zao za kila siku”
Baada ya majibu hayo, Waitara badala ya kuuliza swali la nyongeza kama ulivyo utaratibu na kama alivyotakiwa kufanya na kiti, alisimama na kuanza kulalamika kutoridhishwa na majibu na kutoka nje ya Bunge baada ya kuzozana kwa muda.