Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amesema miundombinu ya barabara, umeme, mawasiliano, maji na reli nchini itadumu kwa muda mrefu ikiwa wajenzi wa miundombinu hiyo watashirikiana wakati wa ujenzi wake.

Ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la tatu la Ustahimilivu wa miundombinu jijini Dar es Salaam, amesema ujenzi wa miundombinu shirikishi ndio suluhisho la miundombinu bora wakati wote.

“Hakikisheni wajenzi wa barabara, reli, umeme, miradi ya maji na mawasiliano mnawasiliana tangu hatua ya mipango ili miundombinu ya aina moja isiharibu miundombinu ya aina nyingine na kuisababishia Serikali gharama zinazojirudia,” amesema Mhe. Waitara.

Ameongeza kuwa taasisi zinazojenga miundombinu zikishirikiana katika hatua zote zinaweza kujenga miradi yao kwa pamoja na kwa gharama nafuu zaidi na hivyo kuondoa usumbufu na uharibifu wa miundombinu.

Aidha amewapongeza kwa kuandaa kongamano la wadau wa miundombinu huku akiwasisitiza kutafuta suluhisho la kudumu katika ujenzi wa miundombinu na kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya kujenga na kuikarabati mara kwa mara.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini, Dk. Bonifasi Nobeji  amesema ushirikishwaji wa wajenzi wa miundombinu unachangia ufanisi katika mnyororo wa thamani katika huduma za uchukuzi na ugavi na hivyo kuisaidia sekta ya bandari kufanya kazi kwa tija.

Rais Samia apokea hati za utambulisho wa Mabalozi 5
Chui amjeruhi mwanamitindo