Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, umekutana na wawakilishi wa serikali ya Taliban kujadili kuhusu uamuzi wa utawala huo, wa kuwazuia wanawake kufanya kazi katika mashirika yasiyo ya kiserikali.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan umesema Kaimu Mkuu wake, Ramiz Alakbarov amekutana na Waziri wa Uchumi wa Taliban, Qari Din Mohammed Hanif kutoa wito kwa kubatilishwa kwa marufuku hiyo.
Hanif alitangaza uamuzi huo mpya, akisema umetokana na madai ya baadhi ya wanawake wanaofanya katika mashirika yasiyo ya serikali hawajifuniki vizuri vazi la Hijab na kwamba shirika lolote litakalokiuka amri hiyo, litafutiwa leseni ya kuhudumu nchini humo.
Hata hivyo, Tangu marufuku hiyo itangazwe tayari mashirika manne makubwa ya misaada ya kimataifa yamesimamisha shughuli zao nchini Afghanistan, yakisema hayawezi kuwafikia watu wenye mahitaji makubwa bila nguvu kazi ya wanawake.