Ili kupata haki zao, Wajane wameiomba Serikali nchini kuwapatia msaada wa kisheria na kusaidiwa huduma ya afya ya akili itakayodhibiti msongo wa mawazo ikiwemo magonjwa ya afya ya akili.
Katibu wa Wajane Taifa, Sabrina Tenganamba ameyabainisha hayo kupitia risala aliyoisoma mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Wajane Duniani, jijini Mbeya.
Amesema, changamoto wanazokumbana nazo Wajane kuwa ni pamoja na kusingiziwa kuwauwa waume zao na kunyang’anywa haki zao za mirathi hivyo, wengi kukabiliwa na umaskini mkubwa na kupelekea msongo wa mawazo hata wengine kujiua.
Akijibu changamoto hizo Waziri, Dkt. Gwajima amesema Serikali itaimarisha zaidi uratibu wa masuala ya Wajane na kusimamia sheria ya msaada wa Kisheria Na. 1 ya mwaka 2017 ili kuhakikisha Wajane wanapata haki zao bila mawaa.