Ujumbe wa Tume inayohamasisha Umoja na Mshikamano na kupambana na aina zote za utengano wa makabila kwa jamii ya watu wa Kenya ( National Cohesion and Integration Commission) umesema kuwa wanatamani kuiona Kenya inakuwa kama Tanzania ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliijenga katika misingi ya umoja na mshikamano.
Wakiongea katika kikao kifupi baada ya ujumbe huo kufanya ziara katika Ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jijini Dar es Salaam, ujumbe huo haukusita kueleza hisia zao juu ya Tanzania na kueleza kuwa suala la Ukabila nchini Kenya bado lipo na ndio moja ya mambo ambayo wanashughulika nayo.
“Tunatamani sana Kenya ingekuwa kama Tanzania, kwani Mwalimu aliijenga Tanzania kuwa taifa moja, tunawaonea wivu, Tanzania imejengwa kama Taifa sisi Kenya bado ni nchi,” amesema Profesa Gitile.
Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga amewaomba katika kuelekea uchaguzi mkuu wahakikishe vyama vya siasa nchini kwao vijiepushe na kuunda makundi ya vijana wa chama “youth league” ambavyo kwa uzoefu uliopatikana katika uchaguzi uliopita nchini Tanzania vikundi hivyo vilianza kujiingiza katika majukumu ambayo sio yao ya kutaka kulinda maeneo ya kupigia kura.
Aidha, Wajumbe wengine waliokuwa katika ziara hiyo ni Kamishna, Profesa Gitile Naituli, Mkurugenzi wa Programu, Millicent Apondi Okatch na Afisa wa elimu ya uraia na uhamasishaji, Richard Nderitu.
Hata hivyo, NCIC ilianzishwa kwa lengo la kuhamasisha umoja na mshikamano katika jamii ya watu wa Kenya kwa kuandaa michakato na sera mbalimbali zinazowezesha kuondoa aina zote za ubaguzi wa kikabila nchini humo.