Leo ni Desemba 25, 2022 ambapo Wakristo Duniani kote wanaungana kusherehekea sikukuu ya kuzaliwa kwa Mwokozi wao Yesu Kristo (Krismasi), kwa kwenda Kanisani na baadaye kuungana pamoja nyumbani na maeneo mengine kwa ajili ya chakula na kutoa zawadi.

Kupitia siku hii, Dar24 imezungumza na waumini mbalimbali kwa nyakati tofauti ambao wametumiana salamu za sikukuu na kutakiana heri, huku wakisisitiza upendo miongoni mwa jamii na kuliombea Taifa. 

Mapambo ya sikukuu ya Krismasi.

Mmoja wa waumini hao, Dickson Motto amesema anamshukuru Mungu kwa mambo mengi aliyowatendea wanadamu kwa mwaka mzima 2022, licha ya mapungufu mbalimbali waliyonayo wanadamu huku akihimiza upendo katika familia.

Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Kanisa la Mtakatifu Stefano Sabaya amesema “Tunaingia katika kipindi kitakatifu cha kufanya tafakari kuhusu kuzaliwa mwokozi wetu Yesu Kristo, yaani maadhimisho ya sikukuu ya Noeli au Christmas hivyo yatupasa kujitafakari juu ya maisha yetu Duniani.”

Kiongozi wa Kanisa la Anglikana akiwasili kwenye Ibada.

Amesema, “Maadhimisho haya ni fursa muhimu ambayo iliwekwa na Kanisa kutoa nafasi ya pekee kutafakari kwa kina fungu la ukombozi kwa mwanadamu baada ya mahusiano yake na Mungu kulegalega, pamoja na hili pia tusiache kuliombea Taifa la Tanzania.”

Awali, mkazi wa Gongolamboto jijini Dar es Salaam, Mahmoud Zubeir amesema “Mimi Kama muislamu naamini katika dini yangu lakini hiyo hainifanyi nisiheshimu dini zingine maana sisi sote ni wa MUNGU na hakuna aliye bora zaidi ya mwingine, ninaomba sikukuu hizi za Krismasi na mwaka mpya tusherehekee kwa amani na utulivu, suala la usalama wetu na familia zetu tulipe kipaumbele.”

Lori lililobeba gesi lawaka moto, 10 wafariki
Askari wawili wauawa mbuga ya Wanyama