Baadhi ya waanchi waliovamia na kugawana shamba la waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye wameanza kujipatia kipato kwa kuuza vipande vya shamba hilo lenye hekari 33 lililoko katika eneo la Mji Mpya, Mwabwepande jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa wa Mji Mpya, Justine Chaganga alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo katika eneo lake huku akieleza bei ya viwanja hivyo. Alisema wananchi hao wameendelea kufanya shughuli katika eneo hilo licha ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki kuwataka waondoke mara moja

“Wapo waliouza kwa shilingi 600,00 na wengine wanauza shilingi 800,000 kulingana na mteja aliyepata. Lakini wengine bado wapo wanashikilia maeneo waliyokatiana,” Chaganga alimwambia mwandishi wa Mtanzania.

 

Sumaye ambaye hivi karibuni alikuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akisumbuliwa na maradhi ya Moyo, alieleza kuwa bado hajafuatilia suala hilo tangu alipotoka hospitalini.

“Nilipoanza kuugua sikufuatilia tena, niliamua nifuatilie hali ya afya yangu kwanza na juzi nimetoka hospitali. Niliona nifuatilie afya yangu kwanza, hayo mengine nitafanya huko mbeleni. Kama kuna watu wanaliuza, sheria itachukua mkondo wake,” alisema Sumaye.

Mwenyekiti wa serikali za mtaa wa Mji Mpya, alieleza kuwa anasubiri agizo la Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ili aweze kuitiha mkutano kati ya wamiliki wa maeneo hayo ili kutatua mapema mgogoro huo ambao unaendelea kuwa mkubwa siku hadi siku. Alisema aliwahi kuagizwa na Makonda kuandaa mkutano lakini baadae alimzuia kwakuwa alipata dharura, hivyo anasubiri agizo hilo tena.

Operesheni Kata Maji yafyeka Nyumbani kwa RPC, Kambi ya Polisi
Serikali yanasa wawekezaji wa madini wakiiba umeme