Wanawake nchini Saudi Arabia wameushangaza uwanja wa mpira wa miguu baada ya kuingia ndani na kushangilia mchezo huo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo.
Historia hiyo imewekwa jana katika mechi moja iliyoshuhudiwa, ingawa sheria ya kuwatenga wanawake na wanaume (wasio waume zao) katika uwanja huo ilitiliwa mkazo katika nchi hiyo ya Kiislamu.
Mashabiki wa mpira wa miguu wanawake waliingia uwanjani mjini Jeddah kupitia mageti maalum ya familia na kukalia viti maalum kwa ajili ya familia.
Tukio hilo lilikuwa sehemu ya ufunguo wa kuvunja baadhi ya miiko dhidi ya wanawake nchini humo katika hatua za kuijenga nchi kuwa ya kisasa.
Jana pia kulionekana dalili nzuri kwa wanawake nchini humo kuanza kuruhusiwa kuendesha gari baada ya kampuni moja ya kuuza magari ilifungua mlango wa mauzo ya toleo maalum kwa ajili ya wanawake.
Kwa mara ya kwanza katika nchi hiyo, wanawake wataruhusiwa kuendesha magari kuanzia mwezi Juni mwaka huu. Hii inafuatia marufuku kali kwa wanawake kuendesha magari iliyowekewa mkazo Septemba mwaka jana.