Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Tabora, Musa Chaulo ametakiwa kuwakamata watu wote wanaohusika na usimamizi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilaya ya Uyui mkoani Tabora kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za mradi huo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amechukua hatua hiyo baada ya kukagua mradi huo na kuonesha kutoridhika na gharama za ujenzi wa baadhi ya majengo ikiwemo kibanda cha mlinzi ambacho ujenzi wake umegharimu shilingi milioni 11.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Septemba 8, 2022 baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA wilaya ya Uyui mkoani Tabora ambapo amesema hajaridhishwa na ujenzi wa chuo hicho ambacho majengo yake yanejengwa kwa gharama kubwa tofauti na uhalisia kwa kutumia mfumo wa nguvu kazi ya ndani (force account).
“Sitamvumilia yeyote atakayemuhujumu Rais Samia Suluhu Hassan, watafutwe na wachukuliwe hatua,” amesema Majaliwa.
Mbali na ujenzi wa kibanda cha mlinzi, pia Waziri Mkuu ameonesha kutoridhishwa na ujenzi wa nyumba za watumishi chuoni hapo ambapo nyumba moja yenye uwezo wa kuchukua familia mbili inajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 114 na tayari wameshatumia zaidi ya shilingi milioni 70 na bado haijakamilika.
“Nyumba moja yenye uwezo wa kuchukua familia tatu Wizara ya Afya inajenga kwa shilingi milioni 90 na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) wanajenga nyumba za walimu zenye uwezo wa kuchukua familia mbili kwa gharama ya shilingi milioni 57 na wanajenga kwa mfumo wa force account kama mnavyojenga hapa, hii haikubaliki,” amesema Majaliwa.
Kutokana na kutoridhishwa na ujenzi wa chuo hicho unaosimamiwa na VETA, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Burian asimamie ujenzi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.