Polisi imesema inawashikilia watu watatu baada ya vifo vya kutatanisha vya vijana 21 mwishoni mwa mwezi Juni katika baa isiyo rasmi Mashariki mwa London, nchini Afrika ya Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Polisi iliyotolewa na Mkuu wa Polisi wa Cape Mashariki, Nomthetheleli Mene imesema waliokamatwa ni pamoja na mmiliki wa baa bubu (54), na wafanyakazi wake wawili, wenye umri wa miaka 33 na 34, na wanazuiliwa kwa tuhuma za kuhusika na usamabzaji wa vileo isivyo halali.
“Kama tumekuwa tukisema muda wote, uchunguzi unaendelea na lazima ufanywe kwa tahadhari na hekima ya hali ya juu ili tuweze kufikia hitimisho tunalotaka,” alisema.
Mmiliki huyo anatarajiwa kufika mbele ya Mhakama Agosti 19, 2022 kwa kosa la kuuza pombe kwa watoto wadogo huku wafanyakazi wake wawili wakiwa tayari wametozwa faini ya randi 2,000 (euro 120) na watafikishwa Mahakamani ikiwa hawataweza kulipa faini hiyo.
Vijana hao 21, wenye umri wa kati ya miaka 14 na 20, walifariki katika mazingira ya kutatanisha katika baa ya Enyobeni iliyopo katika kitongoji cha Scenery Park Mashariki mwa London.
Miili mingi ilipatikana kwenye baa hiyo bila majeraha yoyote, lakini baadhi yao walifariki ndani ya saa chache mara baada ya kufikiswa hospitalini.
Mamlaka ilikuwa imedokeza kuwa huenda vifo hivyo vilisababishwa na mkanyagano, lakini wiki mbili baada ya mkasa huo uchunguzi wa vipimo ulishindwa kubainisha chanzo cha vifo.
Walionusurika wanasema kulitokea harufu nzito iliyofanya washindwe kupumua na kudai kuwa huenda kuna mtu alipuliza hewa ya sumu.