Watoto wawili wa Donald Trump wamekataa kutoa ushahidi wa uchunguzi wa ulaghai katika biashara ya familia hiyo.
Donald Jr, 44, na Ivanka, 40, waliamriwa kutoa ushahidi na Mwanasheria Mkuu wa New York Letitia James, ambaye alifungua uchunguzi wa kiraia 2019 kwa madai kwamba – kabla ya kuchukua ofisi, Trump alikuwa ameongeza thamani ya mali yake kwa benki wakati akitafuta mikopo.
Mawakili wa Trump wanajaribu kumzuia wakili huyo, James, kumhoji rais huyo wa zamani wa Marekani na watoto wake wakimwomba jaji kufuta ombi walilotaja kama lisiyokuwa la kawaida na lisilo la kikatiba ya kutoa ushahidi wao.
Trump alimshtaki wakili James mwezi uliopita, akimshutumu mwanasheria mkuu mteule wa Democrat kwa kutekeleza uwindaji uliochochewa kisiasa dhidi yake, ambaye ni mwanachama wa Republican.
Ombi la Mahakama lililowasilishwa Jumatatu ni mara ya kwanza kwa wachunguzi kusema wanataka kuwahoji Donald Jnr na Ivanka chini ya kiapo.
Mtoto mwingine, Eric, 37, ambaye ni makamu wa rais mtendaji katika Shirika la Trump, alihojiwa mnamo Oktoba 2020.
Kesi ya madai ya Bi James ni tofauti na uchunguzi wa jinai unaoendelea huko Manhattan kuhusu shughuli za kibiashara za shirika hilo.
Donald Jr na Eric walichukua udhibiti wa kampuni hiyo pamoja na Allen Weisselberg, afisa mkuu wa fedha, wakati baba yao alipoingia madarakani Januari 2017.
Ivanka pia alifanya kazi katika Shirika la Trump, kabla ya kuwa mshauri mkuu wa White House.