Mamlaka za Usalama nchini Nigeria, zimesema takriban watu 30 wameuawa katika shambulio dhidi ya kambi ya wakimbizi wa ndani kaskazini-kati mwa Nigeria, likiwa ni shambulio la pili kwa ukubwa katika eneo hilo wiki hii.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Afisa wa Polisi Benue, Sewuese Anene amesema watu watu hao wakiwa na silaha waliwashambulia raia katika kijiji cha Mgban kilichopo katika jimbo la Benue siku ya Ijumaa jioni (Aprili 7, 2023), na uchunguzi unaendelea.
Amesema, ingawa haijulikani ni nani aliyehusika na shambulio hilo, mamlaka ilisema tuhuma iliangukia kwa wafugaji wa eneo hilo ambao walipigana siku za nyuma na wakulima kuhusu migogoro ya ardhi kaskazini-kati mwa Nigeria.
Aidha, wakulima hao wanawatuhumu wafugaji hao, wengi wao wenye asili ya Fulani, kwa kulisha mifugo yao kwenye mashamba yao na kuharibu mazao yao. Wafugaji hao wanasisitiza kuwa mashamba hayo ni njia za malisho ambazo ziliungwa mkono kwa mara ya kwanza na sheria mwaka 1965, miaka mitano baada ya nchi hiyo kupata uhuru wake.
Ghasia hizo, zinakuja siku chache baada ya watu wenye silaha kuua takriban watu 50 katika mashambulizi mawili tofauti kwenye kijiji cha Umogidi katika jimbo hilo, ambalo linajulikana kama “kikapu cha chakula cha Nigeria” kwa sababu ya mavuno mengi. Vijiji hivyo viko umbali wa kilomita 170 (maili 105) kutoka kwa shambulio la Ijumaa, hata hivyo, haijulikani ikiwa kundi moja lilihusika na mashambulizi yote mawili.