Takribani watu 805, wakiwemo wafungwa, watumishi wa magereza pamoja na familia zao katika Gereza la Bukoba Mkoani Kagera wamefikiwa na elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa Marburg.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Dkt.Tumaini Haonga baada ya kutembelea gerezani hapo kutoa elimu namna ya kujikinga na Marburg, Mwakilishi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya, Beauty Mwambebule amesema ni muhimu kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Beauty Mwambebule akitoa elimu jinsi ya kujikinga na Marburg katika gereza la Bukoba mkoani Kagera.

Amesema, “Kinga ni bora kuliko tiba ; wakati mwingine inaweza kuchukua kuanzia siku 2 hadi 21 kuonesha dalili mfano homa, kutapika, kuharisha damu au kutapika damu ni muhimu tuchukue tahadhari mapema.”

Kwa upande wake Mtaalam wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Jackline Saulo amesema ni muhimu kuepuka misongamano isiyo ya lazima na kusema tayari maelekezo yameshatolewa kuhakikisha sehemu zote zenye mikusanyiko ya watu kunakuwa na vifaa maalum vya kunawia mikono.

Mmoja wa Maafisa gereza la Bukoba akipokea bango la uelimishaji kuhusu ugonjwa wa Marburg.

Akitoa neno la shukrani, Mkaguzi wa Jeshi la Magereza, Fredrck Katabazi na Mkaguzi Msaidizi, Venance Vedastus wa Gereza la Bukoba wametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kuwa mstari wa mbele kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mara yanaporipotiwa na kuongeza wigo wa uelimishaji.

Watalaam wa Afya kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera, wameendelea kutoa elimu jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuwafikia viongozi wa dini, waendesha pikipiki, maduka na sehemu zote za kutolea huduma na mikusanyiko.

Trilioni 8.64 kuendeleza miradi saba ya vipaumbele nchini
Amir Khan astaafu masumbwi kwa aibu