Takribani watu sita wameuawa na wengine 200 wamejeruhiwa katika maandamano ya kupinga ushindi wa awamu  ya pili wa Rais wa Indonesia, Joko Widodo.

Maandamano hayo yalianza kwa amani Jumanne wiki hii na baada ya saa kadhaa waandamanaji walianzisha vurugu kwa kuchoma moto magari na kuwarushia baruti polisi ambao walianza kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Maafisa wa Polisi walishindwa kuthibitisha idadi ya waathirika wa maandamano, lakini Gavana wa Mji mkuu wa nchi hiyo, Jakarta, Anies Basedan alitaja watu sita kupoteza maisha na 200 kujeruhiwa. Maafisa hao wa polisi walieleza kuwa bado hawajathibitisha idadi halisi lakini walikiri wana taarifa za watu waliopoteza maisha na kwamba wataeleza baada ya miili kufanyiwa uchunguzi na madaktari.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Polisi nchini humo, tayari wanawashikilia watu 69 kutokana na vurugu za maandamano ya kupinga ushindi wa Rais Widodo.

Maandamano hayo yalianza baada ya Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kutangaza matokeo yaliyomtaja Rais Widodo kuwa mshindi kwa asilimia 55.5 ya kura dhidi ya mpinzani wake wa muda mrefu, Prabowo Subianto .

Hii sio mara ya kwanza kwa Rais Widodo kumshinda mpinzani wake Prabowo. Mwaka 2014, Rais huyo alishinda lakini mpinzani huyo pia alilalamika kuhusu udanganyifu kwenye uchaguzi huo.

Zaidi ya watu milioni 192 walithibitishwa kupiga kura ya kumchagua Rais wa Indonesia katika uchaguzi uliofanyika Aprili 17 mwaka huu, na baada ya matokeo kutangazwa jana, maelfu ya wafuasi wa Prabowo waliokuwa nje ya jengo la Tume ya Uchaguzi walianza kuzunguka kwenye mji wa Jakarta kupinga matokeo hayo.

Msemaji wa jeshi la Polisi wa nchi hiyo amesema usalama unaendelea kuimarishwa na zaidi ya polisi 30,000 wapo mjini kulinda usalama wa raia na mali zao.

 

 

 

 

 

Lissu atangaza tarehe ya kurejea Tanzania, mapokezi yake
Simba kufanya maajabu dhidi ya Sevilla? Tutazame mtaji walionao