Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema watumishi wa 12 wa Baraza la Mitihani wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuvujisha mitihani ya kidato cha nne, katika shule ya Sekondari ya Twiboki.
Prof. Mkenda ameyasema hayo hii leo Februari 9, 2023 Bungeni Jijini Dodoma, wakati akitolea ufafanuzi wa mwongozo uliyo ombwa na Mbunge wa Bunda Mwita Gitere, aliyetaka kufahamu watoto 66 waliofutiwa matokeo ya kidato cha nne katika shule ya Twiboki hatua gani zimechukuliwa kwa waliovujisha mitihani na wasimamizi wa mithiani hiyo.
Alisema, “Ni vizuri wote tuwe makini katika suala la mitihani na udanganyifu kwa ujumla wake, tunapozungumza ubora wa elimu ni pamoja na kuhakiki wale wanaofanya ‘transition’ kwa kuchujwa kupitia mitihani iwe inafanyika kwa ukweli.”
”kilichotokea katika shule hiyo ya Twiboki iliyopo mkoani Mara ni kwamba kuna sababu za kutosha kulikuwa na udanganyifu katika mitihani, majibu yanafanana ambayo ‘statistically’ haiwezekani yakafanana” amesema
“Kama wizara tumehakiki, swali la msingi kama ni hivyo kulikuwa na watu wanasimamia iwezekanaje wawe na majibu yanayofanana bila ‘coordination’ ni hatua gani inachukuliwa? Mbona mmoja matokeo yake yametangazwa wengine wote hawakutangazwa?
“Hatua zilizochukuliwa nimepewa taarifa jana kuwa watu 12 wapo mahabusu kwa sababu za kuvujisha mitihani na hao wapo na connection na shule hii ya Mara. Na uchunguzi unaendelea kujua nini kilitokea mpaka wanafunzi wakawa na majibu yanayofanana.”Amesema Mkenda.
Mkenda amesema, pia wapo kwenye uchunguzi wa shule ambayo imefungua kabrasha za mitihani mapema kabla ya muda na kujibu maswali na wanafunzi katika Bwalo la Chakula na badae ndio wakawaingiza katika vyumba vya mitihani.
“Sasa hili la mtoto mmoja ambaye amepewa matokeo yake hatujui kama hakuonyeshwa mtihani au alionyeshwa akafanya kwa njia anazozijua yeye, tupo tayari kukutana na wazzi kama wanahisi Watoto wao wameonewa.
Itakumbukwa, Kaimu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) Athumani Amas, alisema kuwa kati ya wanafunzi hao, 66 wamefutiwa matokeo kwa sababu wamefanya udanganyifu na kwa mujibu wa Necta, ni mwanafunzi mmoja tu mwenye matokeo aliyepata daraja la kwanza la pointi nane.
Wanafunzi hao 66 waliofutiwa matokeo ni sawa na asilimia 20 ya wanafunzi 333 ambao wamefutiwa matokeo katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022.