Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uingereza Wayne Rooney, amesema hatokatishwa tamaa na changamoto zinazomkabili kwa sasa na badala yake ataendelea kupambana ili aweze kurejea katika kiwango chake.

Rooney amesema anatambua changamoto kubwa iliyo mbele yake kwa sasa ni kucheza soka la ushindani kama ilivyokua siku za nyuma, na hatua ya kuanzia benchi katika mchezo wa hii leo dhidi ya Slovenia anaichukua kama sehemu ya mapambano ya kuhakikisha anafanya jitihada zaidi.

Jana jioni kocha wa muda wa timu ya taifa ya Uingereza Gareth Southgate alidokeza taarifa za kutotarajia kumtumia mshambuliaji huyo wa Man Utd katika mchezo wa hii leo, kutokana na kiwango alichokionyesha wakati wa mchezo ddidi ya Malta mwishoni mwa juma lililopita kutomridhisha.

Tayari kocha huyo ameshamkabidhi majukumu kiungo wa Liverpool Jordan Henderson ya kuwa nahodha wa kikosi cha Uingereza kwa ajili ya mchezo dhidi ya Slovenia, badala ya Rooney.

Katika hatua nyingine Rooney, ameendelea kusisitiza suala la kutaka kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya Uingereza mara baada ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, hivyo anaamini kwa muda uliosalia atakuwa na nafasi nzuri ya kupambana na kurejesha uwezo wake.

“Wakati mwingine mambo huenda tofauti, naamini nitafanikisha ahadi ya kuacha kuichezea timu hii mara baada ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, kwa kujumuika na wenzangu kwa ajili ya kuiwezesha Uingereza itinge kwenye fainali hizo. Kwa sasa nina umri wa miaka 30 ambao unaniwezesha kufanya kila niwezalo ili niziepuke changamoto zinazonikabili.” Amesema Rooney.

Paul Pogba Aibeba Ufaransa, Awatumia Salamu Waliombeza
Mahakama Kuu yaridhia CUF kufungua kesi dhidi ya Lipumba, Msajili