Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ameikana orodha ya majina ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini ikiwa ni siku chache baada ya kuagiza jeshi la polisi nchini kumkabidhi orodha hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufanya kikao na maafisa wakuu wa Jeshi la Polisi nchini katika makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam, Kitwanga alieleza kuwa orodha ya majina ya wauza madawa ya kulevya haitasaidia kukomesha biashara hiyo na badala yake ni vyema kuunda mfumo thabiti wa kudhibiti uingiaji wa dawa hizo nchini.

“Kuwa na orodha haiwezi kusaidia, tumejadiliana  namna ya kuweka mfumo mzuri wa kudhibiti uingizwaji na uuzwaji wa dawa za kulevya,” alisema waziri Kitwanga.

Aidha, Waziri Kitwanga alisisitiza kuwa yeye hajawahi kuwa na orodha ya majina ya vigogo wa dawa za kulevya na kuongeza kuwa hata angekuwa na orodha hiyo haitasaidia kupambana na biashara hiyo haramu.

“Mimi sina ‘list’ (orodha) na sijui kama Rais anayo, nashangaa nyie (waandishi wa habari) mnaandika tu na hata ningekuwa nayo haisaidii kitu maana hatuwezi kwenda kumkamata mtu na kumshtaki bila kuwa na ushahidi,” alisema.

Wakati wa utawala wake, rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema kuwa anayo orodha ya majina ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya. Hata hivyo, hakuwahi kuweka hadharani majina hayo.

 

Walichozungumza Rais Magufuli na Maalim Seif walipokutana Ikulu Jana
Sakata la TBC1: Je wajua ni kosa TV kurusha Tangazo la Biashara kwenye Taarifa ya Habari? Soma hapa