Serikali ya Afrika Kusini imeeleza kuumizwa na hatua ya tovuti ya nchini Rwanda kumtaja Waziri wake wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuwa ni ‘kahaba’.
Kwa mujibu wa Serikali ya Afrika Kusini, tovuti hiyo inayodaiwa kuwa inaunga mkono Serikali ya Rwanda iliandika kwa kukosoa uamuzi wa Waziri huyo wa Afrika Kusini, Lindiwe Sisulu kukutana na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Rwanda, Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa ambaye alikimbilia uhamishoni jijini Johannesburg.
Mvutano huo ulianza baada ya Waziri Sisulu kueleza kuwa alipokutana na Jenerali Nyamwasa alishangaa kuelezwa kuwa Jenerali huyo yuko tayari kuzungumza na Serikali ya Rwanda ili kufikia maridhiano.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe alitumia mtandao wa Twitter kukosoa vikali mkutano kati ya Waziri Sisulu na Jenerali Nyamwasa akieleza kuwa kama Serikali ya Afrika Kusini imeamua kukutana na Jenerali huyo ambaye kwao ni mtu mwenye hatia anayestahili kufungwa waelewe kuwa Rwanda haitahusika kwa namna yoyote na mazungumzo hayo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Ndivhuwo Mabaya amesema kuwa Balozi wa Rwanda nchini humo ameitwa jijini Pretoria kwa ajili ya mazungumzo kuhusu tovuti ya nchi hiyo kumuita waziri wake ‘kahaba’.
Kadhalika, Mabaya amesema kuwa Balozi wa Afrika Kusini nchini Rwanda ameitwa kurejea nyumbani mara moja.
Tovuti hiyo ya Rwanda ilifuta habari hiyo lakini Afrika Kusini imeendelea kueleza kuwa haiwezi kuvumilia kuona lugha isiyo ya kidiplomasia inatumika dhidi ya kiongozi wake.
Mgogoro wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Afrika Kusini una muda mrefu, ikumbukwe kuwa mwaka 2014 Afrika Kusini iliwafukuza wanadiplomasia watatu wa Rwanda kutokana na shambulizi katika nyumba ya Jenerali Nyamwasa jijini Johannesburg. Rwanda ilijibu kwa kuwatimua wanadiplomasia sita wa Afrika Kusini.
Jenerali Nyamwasa aliwahi kuwa mkuu wa jeshi la Rwanda kuanzia mwaka 1998 hadi 2002, lakini pia mkuu wa kitengo cha intelijensia ya nchi hiyo. Na baadaye alikuwa balozi wa Rwanda nchini India kati ya mwaka 2004 na 2010.
Februari 2010, Jenerali Nyamwasa ambaye alikuwa miongoni mwa waasisi wa chama tawal cha Rwanda cha Rwandan Patriotic Front alikimbilia nchini Afrika Kusini akitokea nchini India ambapo aliomba nafasi kuwa uhamishoni. Serikali ya Rwanda ilimfungulia mashtaka nchini kwake kwa madai ya kushiriki katika tukio la kigaidi la mabomu matatu mwaka huo jijini Kigali.
Ingawa Rwanda iliomba Serikali ya Afrika Kusini kumkatamata, haikuwezekana kutokana na kutokuwepo makubaliano ya ushirikiano wa aina hiyo.