Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema serikali visiwani humo imejipanga kumaliza kesi za ulawiti na vitendo vya jinai ambazo zimekua zikitokea kwa kasi kutokana na vificho vinavyofanywa na ndugu wa familia wanaotendeana vitendo hivyo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Dar24 ofisini kwake, Mazrui amesema serikali ya Rais Hussein Mwinyi imetenga mahakama ya peke yake inayohukumu kesi hizi, na kwamba zimewekwa sheria kali na kutoa kutoa elimu kwa vijana wadogo na watoto wa rika ambao ndio waathirika wakuu.
“Tuna shida kubwa kwa mfano, mwaka uliopita ni zaidi ya 1000 na mia nne(1400), za kulawiti ni kama mia nne, kubaka watoto mia nne na kitu, kupiga wanawake kama mia tatu na kitu kwa hivyo kesi zipo ambazo zinatuathiri sana. Lakini sasa hatuna tena masikhara, Mahakama imewekwa peke yake, sheria imekazwa, elimu tunaitoa kwa kasi, polisi kusaidiana na wazee kusuluhisha kesi na kuhukumu hizi kesi katika vituo vya polisi…manaake sana wanaofanya mambo haya ni ‘family members’, Mtu akishaona huyu mwanangu kalawitiwa na Amy yake itakua fitna. Sasa, sasa hivi usiposema wewe Mzee utakwenda wewe, lazima heshma iwepo na hatuwezi kuendelea na hiyo ‘situation’ hayo mambo yote tunayamaliza mwaka huu huu,” amesema Waziri Mazrui.
Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika linaloshughulikia watoto UNICEF, mtoto mmoja kati ya 10 wa kiume hukumbana na udhalilishaji wa kingono, na mmoja kati ya watoto wa kike 20 nae hukumbumbana na udhalilishaji wa kingono Zanzibar.
Aidha, Waziri Mazrui amesema katika kuongeza upatikanaji rahisi wa huduma za afya kwa wananchi wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanziba kwa mwaka 2022 inaanzisha utaratibu wa mfumo wa bima ya afya ili kukabili tatizo la huduma za afya bila malipo na itakayokuwa yenye kukidhi viwango vya huduma kwa kila mwananchi.
Amesema watakaoanzia kupata huduma za bima ya afya ni wafanyakazi wa sekta zote za serikali na sekta binafsi ili kusaidia kupunguza gharama kwa serikali za kuhudumia wananchi wote huduma za afya bure.
Waziri Mazrui amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inatoa huduma za afya bila malipo tangu mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, lakini serikali kutokana na hali ya uchumi kuwa ngumu kwa sasa baadhi ya vituo vya afya vinakosa huduma zote hivyo wananchi wanachangia huduma kwa kupata matibabu sehemu tofauti kila moja kwa kituo chake.
“Tumeona kwamba ni mzigo mkubwa kwa serikali kwa kweli kwa sababu uchumi umekua mgumu, kwa sababu Zanzibar bado tunazaa sana kwa kweli, ongezeko la watu ni kubwa mno, na bado hatujaweza kuwa ‘control’ watu wasizae watoto wengi. Lengo lilikua mpaka 2020 lengo la kuzuia watu kuzaa sana ilikua 20% lakini mpaka sasa 2022 ni 14%, kwa sababu bado watu wanaamini kuwa Rizki anatoa Mungu na kucontrol uzazi ni haramu na nini…kwa hiyo utakuta tunazaa sana, maskuli yanafurika, mahospitali yanafurika,” alisema.
“Kazi ya uzazi ni kubwa kwa idara ya afya, mimba tuilee mpaka uzae mtoto, na mimba isipolelewa vizuri utazaa mtoto njiti, na mtoto njiti lazima tumlee mpaka awe mtoto kweli. Kwa hivyo tunasema suala la afya ni bure hawalipi chochote kile.” Alisema Mazrui
Akizungumzia swala la UVIKO 19, Waziri Mazrui amewaasa wananchi wote kupata chanjo ya ugonjwa huo ili kujikinga na hasa ikitegemea kuwa mtu aliechanjwa mwili wake unapigana tofauti na mtu ambae hajachanjwa.
Amesema yeye binafsi amepata maambukizi ya UVIKO 19 na ameweza kupona kwa haraka kutokana na kupata chanjo alizozipata awamu zote mbili.
“Zipo sehemu nyingine ngumu zaidi kutoa elimu ya chnajo, mnafika mnaongea weee mkimaliza wanachnaja watano, lakini nawaambia wale waelimishaji, msikate tamaa, pale mlipoishia jana basi leo muamkie hapo na nguvu mpya. nashukuru Mungu chanjo tunzo za kutosha, na watoa chanjo wanatosha hivyo watu waamke wapate chanjo inasaidia,” alisema.
Waziri Mazrui amesema kwa sasa hali ya maambukizi ya UVIKO 19 katika visiwa vya Zanzibar sio mbaya kwa sababu mpaka sasa tangu kuingia kirusi cha Omicron wengi wanapona na vifo vitatu tu vimetokea.
“Mipaka yetu hatujaifunga ila lazima tuwe salama, tumehakikisha kwamba kila mgeni anayeingia nchini ana test ya masaa mawili kabla ya kuingia Zanzibar na akifika Airport tunampima ‘Rapid Test’…wengi wanaokuja hapa kwetu wanakuja wameshachanjwa na wengi wanakuwa negative, lakini tukimkuta mtu ana maambukizi tunamu ‘isolate’ anakaa huko kwa siku 7 na baada ya hapo anapimwa tena. Kwa hivyo sisi kuchanjwa hapa ni moja katika nyenzo za kujenga uchumi wetu.” Waziri Mazrui.
Mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Zanzibar (MKUZA) ni pamoja na kuimarisha huduma za Afya kwa kila mwananchi.