Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amewataka waajiri wote nchini kutonyanyasa wanawake katika masuala ya kazi ili kuwa na usawa maeneo ya kazi.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akifungua semina ya siku moja ya viongozi wanawake kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini walipokutana kujadili masuala yanayowahusu wawapo kazini ikiwemo, haki na wajibu wao wawapo kazini.
Amesema kuwa waajiri hawana budi kubadili mitazamo hasi iliyopo katika jamii ya kuona wanawake ni viumbe dhaifu na wenye majukumu mengi yanayoweza kukwamisha jitihada zao wawapo kazini badala yake wawaone kuwa ni viungo muhimu katika kuchangia uzalishaji na maendeleo nchini.
“Mchango wa wanawake ni mkubwa endapo utatambuliwa na kuthamini katika nyanja zote za ukuaji wa uchumi, hivyo ni vyema maeneo ya kazi waajiri watimize wajibu wao kwa kundi hili kwa kuzinigatia sheria zilizopo na wasinyanyaswe na waendelee kuheshimiwa na kupewa haki na stahiki zao kama wafanyakazi wengine.”amesema Mhagama.
Aidha, amewataka wanawake kuendelea kuvitumia vyama vya wafanyakazi kama jukwaa maalum la kueleza na kutatua changamoto zao.
Naye rais wa Shirikizo la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amempongeza waziri pamoja na changamoto zilizopo katika kufikia haki sawa kwa wote, huku akielezea umuhimu wa kuendelea kuliinua kundi hilo ili kuwasaidia wanawake wa Kitanzania katika kupata haki na usawa kwenye maeneo yao ya kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti Kamati ya Wanawake Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Rehema Ludanga amesema kuwa, ni wakati sahihi kuendelea kuchangamkia fursa za maendeleo ikiwemo uanzishwaji wa viwanda vya wanawake vitakavyosaidia kuondokana na hali ya utegemezi na kuchangia katika ongezeko la uzalishaji nchini.