Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini waongeze ubunifu wa kusukuma ajenda za Serikali kwa umma na si kusubiri kazi zifanywe na Waandishi wa Habari wengine.

Majaliwa, ametoa wito huo leo Machi 27, 2023 wakati akifungua kikao kazi cha 18 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kilichoanza leo katika Kituo Cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema, “mnapofanya kazi ongezeni ubunifu wa kusukuma ajenda za Serikali kwa umma na msisubiri kazi zifanywe na wanahabari wengine. Hakikisheni kila mwananchi anapata elimu na taaarifa sahihi kuhusu faida na umuhimu wa miradi na mipango au shughuli zinazotekelezwa na Serikali.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema, “maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini mnao wajibu wa kuhakikisha kuwa yale yote yanayopangwa na kutekelezwa na Serikali yanafahamika kwa umma wa Watanzania kwa usahihi, kwa wakati na kwa tija.”

Aidha ameongeza kuwa, wanapofanya mawasiliano hasa ya kimkakati, wahakikishe wanafahamu lengo la mawasiliano wanayotaka kufanya, faida na matarajio ya kutekeleza mawasiliano husika, nani mlengwa wa mawasiliano hayo pamoja na kuchagua njia sahihi za mawasiliano.

Ili kuwawezesha maafisa hao kutekeleza majukumu yao, Waziri Mkuu pia amewaagiza Makatibu Wakuu wote, Wakurugenzi wa Halmashauri na taasisi zote za umma watenge bajeti ya kutosha kugharamia shughuli za utoaji wa taarifa pamoja na elimu kwa umma na kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa kwa tija na ufanisi uliokusudiwa.

Watafiti watakiwa kuweka mipango matumizi rasilimali za Bahari
Wizara ya Maji yawasilisha taarifa kwa Kamati ya Bunge