Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Nyetanyahu leo ametua nchini Uganda kuanza ziara ya siku nne kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika Mashariki ikiwa ni mara ya kwanza kwa Waziri Mkuu wa Israel kutembelea bara la Afrika zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Nyetanyahu ametua katika uwanja wa ndege wa Entebe na kukumbuka tukio la kishujaa lililofanywa na makomando wa Israel mwaka 1976, waliofanya oparesheni ya uvamizi na kuwaokoa mateka wa nchi hiyo waliokuwa wameshikiliwa na askari wa Palestina waliokuwa wanaungwa mkono na aliyekuwa rais wa Uganda, Idi Amin Dada.

Akizungumza katika uwanja wa Entebe, Waziri Mkuu huyo wa Israel amesema kuwa tukio hilo lililochukua maisha ya kaka yake Yonatan aliyekuwa akiongoza operesheni hiyo usiku wa manane na kuuawa kwa kupigwa risasi, lilibadili maisha yake. Kifo cha kishujaa cha kaka yake katika tukio hilo ndicho kilichomfanya Benjamin aanze kuonekana zaidi na kuanza kuifuata ndoto yake ya kuwa kiongozi wa nchi hiyo.

“Hii ni siku nzuri kwangu. Miaka 40 iliyopita wanajeshi wa Israel walitua katika usiku wa mauaji ndani ya nchi ambayo ilikuwa inaongozwa na dikteta aliyewapa hifadhi magaidi. Leo, tumetua mchana katika nchi ya kirafiki inayoongozwa na rais anayepambana na magaidi,” alisema Nyetanyahu.

Nyetanyahu ameahidi Israel kushirikiana na Uganda katika kusaidia kukabiliana na ugaidi.

Naye Rais Yoweri Museveni alimshukuru Nyetanyahu kwa kuizulu nchi hiyo na kuahidi kushirikiana Israel katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama dhidi ya vitendo vya kigaidi.

Nyetanyahu anatarajia kutembelea pia nchi ya Kenya, Rwanda na Ethiopia kabla hajarejea nchini kwake.

Kitwanga afunguka kuhusu kutumbuliwa na JPM, Sakata la Lugumi
Makonda Awaapisha Wakuu Wa Wilaya Mkoa Wa Dar es salaam