Vinara wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba wamesisitiza kuendeleza moto wa kufanya vyema katika mchezo wao wa leo ambao utawakutanisha na Mbao FC katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Uongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi umesema haupo tayari kuona kikosi chao kikipoteza point hata moja katika mchezo huo na michezo mingine, hivyo wamehakikisha hamasa inaendelea kwa wachezaji wao ambao wana jukumu la kuifikisha Simba katika mafanikio msimu huu.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara amesema japokuwa Mbao FC inacheza ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa mara ya kwanza, lakini hawataidharau.

“Hatupaswi kubweteka kwa matokeo mazuri ya sasa, tunatakiwa tuendelee kufanya vizuri, tusipoteze hata pointi moja. Hatutaki hata droo, lazima tushinde kila mechi, ili tuendelee kuwaacha washindani wetu katika mbio za ubingwa (Azam na Yanga),”alisema.

Hajji amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi leo Uwanja wa Uhuru kuisapoti timu yao ikimenyana na Mbao inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu kihistoria.

Simba SC ambayo imeweka kambi Ndege Beach Hotel, Mbweni, Dar es Salaam, ikijifua Uwanja wa Boko Veterani, itaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar mabao 2-0 Uwanja huo huo wa Uhuru.

Simba SC inagongoza katika msimamo wa ligi kuu ikiwa imejikusanyia pointi 23 baada ya kucheza mechi tisa, ikifuatiwa na Stand United ya Shinyanga yenye pointi 20 za michezo 10, wakati mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 18 za michezo tisa ni ya tatu.

Dk Slaa aibukia Sakata la Gambo na Lema, amkingia kifua Lema
Ulikua Usiku Wa Kibabe, Miamba Ya Ulaya Yaunguruma