Wimbo wa taifa wa Ufaransa, La Marseillaise, utachezwa kabla ya mechi zote za Ligi ya Premier wikendi hii kuanza, wasimamizi wa ligi hiyo wamesema.
Wimbo huo utachezwa baada ya sarafu kurushwa kuamua nani ataanzisha mchezo, huku wachezaji wa timu zote mbili wakikusanyika kwenye mduara katikati ya uwanja pamoja na marefa.

Afisa mkuu mtendaji wa Ligi ya Premia Richard Scudamore amesema hatua hiyo ni ya kuunga mkono Ufaransa na kutoa heshima kwa wahasiriwa baada ya mashambulio ya Paris yaliyoua watu 129 Ijumaa iliyopita.

Wimbo wa La Marseillaise pia ulichezwa wakati wa mechi ya kirafiki kati Uingereza na Ufaransa Jumanne. Uingereza walishinda mechi hiyo.

Kuna wachezaji 72 kwa sasa Ligi ya Premia wanaotoka Ufaransa.

“Ukizingatia ushirika wetu, pamoja na uhusiano wa karibu ambao umekuwepo kati ya Ligi ya Premia na Ufaransa, kucheza wimbo wa La Marseillaise kuonyesha kwamba tuko pamoja nao ndilo jambo bora kufanya,” alisema Scudamore.

Chelsea tayari wametangaza wachezaji wao watavalia tepe za rangi nyeusi mikononi zenye michoro ya bendera ya Ufaransa wakati wa mechi yao ya nyumbani dhidi ya Norwich City Jumamosi.

Newcastle United pia watafanya vilevile wakati wa mechi yao ya nyumbani dhidi ya Leicester City.
Ligi ya Premia imewasiliana na klabu zote kuhusu tahadhari na kuzishauri kuhusu usalama.

Federer, Nadal Mwendo Mdundo
Lipumba amshauri Magufuli kuhusu Bajeti na hali ya Zanzibar