Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema imebaini uwepo wa watu wenye nia ovu (matapeli) wanaosambaza taarifa za uongo za kutangazwa kwa nafasi za ajira katika sekta ya Afya na kutumia barua pepe inayosomeka; specialrecruitment.afya.go.tz@gmail.com ambao wanatumia anuani hiyo kuwatapeli wananchi wenye uhitaji wa ajira kuwa Wizara imetangaza ajira na kuwaomba watume maombi kupitia anuani hiyo na kutuma kiasi fulani cha fedha ili maombi yao yazingatiwe.

“Tunaomba ifahamike kuwa anuani hiyo sio ya Wizara ya Afya bali ni Matapeli wanaotaka kuwaibia Wananchi, anuani rasmi ya Wizara kwa barua zote ni: Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Afya), Mji wa Serikali Mtumba, Barabara ya Afya, S.L.P 743, 40478 DODOMA – TANZANIA na Baruapepe: ps@afya.go.tz” imeeleza taarifa ya Wizara ya Afya.

“Tunawaomba Wananchi kuzingatia vyanzo rasmi vya Wizara kufuatilia na kujiridhisha na matangazo sahihi ya ajira za sekta ya afya pamoja na njia za uwasilishaji maombi kupitia tovuti ya Wizara: www.moh.go.tz pamoja na kurasa zetu rasmi za mitandao ya jamii Instagram, Facebook, Tweeter zinazosomeka: wizara_afyatz na MsemajiAfyaTz kuepuka utapeli unaofanywa na watu wasio wema,” imeongeza taarifa hiyo.

Aidha, Wizara imeeleza kuwa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na mamlaka za udhibiti wa mawasiliano ya kimtandao nchini, wanaendelea kuwafuatilia wanaotoa taarifa hizo na kutumia anuani zisizo rasmi kufanya utapeli kwa wananchi na mara watakapobainika watafikishwa katika mkono wa Sheria.

Rais Samia kupokea ripoti za CAG, TAKUKURU leo
NEC yatangaza Uchaguzi mdogo Muhambwe