Shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Kagera limekabidhi msaada wa madawati 350 yenye thamani ya shilingi millioni 28 kwa shule za msingi za Ruzila, Kabilizi, Bituntu na Kamkole zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ili kurahisisha watoto kusoma vizuri.

Shirika hilo limetoa msaada huo kama sehemu ya kuadhimisha miaka 40 tangu kuingia kwake nchini.

Akikabidhi Madawati hayo, Kaimu Mratibu wa mradi wa Rukoma, Victor Nsiima amesema kuwa mbali na shirika hilo kujitahidi katika kutoa huduma za kuisaidia jamii kujikwamua kiuchumi, wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika katika sekta za Afya, Kilimo, Ufugaji, Maji pamoja na Elimu ili kumtengenezea mtoto mazingira rafiki ya maisha.

Aidha, ameongeza kuwa Shirika hilo linakabiliana na changamoto za kuwepo kwa mimba za utotoni zinazoathiri malengo ya shirika kutaka kila mtoto apate elimu, licha ya jamii kuwa na kipato kidogo hali inayopelekea kushindwa kumudu gharama za maisha.

Diwani wa Kata Rukoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Murushid Ngeze ameeleza kuwa awali kabla ya Shirika la Word Vision kuwajengea vyumba vya madarasa na kuwaletea madawati, shule ya Msingi Ruzila ilikuwa na vibanda vilivyotumika kama madarasa na chumba kimoja kilikuwa na mbao mbili za kufundishia.

Kutokana na hali hiyo wanafunzi walikuwa wanalazimika kusoma madarasa mawili ndani ya chumba kimoja wakikaa kwa kupeana migongo huku masomo yakiendelea.

Ngeze amelishukuru shirika hilo na kuliomba kuendelea kusaidia maeneo mengine yenye uhitaji.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawiro amelishuru shirika la Word Vision Rukoma kwa ushirikiano mzuri na serikali katika kuhakikisha serikali inatimiza adhma yake ya kutoa elimu bila malipo na kuitaka jamii kuendelea kujitoa na kulinda miundombinu wanayoletewa na serikali pamoja na wafadhili ili iweze kudumu na kuwasaidia watoto wao hapo baadae.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 7, 2021
RC Dar ataka mahitaji ya wananchi kupewa kipaumbele