Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umeweka wazi kuwa hauna maneno mengi zaidi ya kuhitaji alama tatu za TP Mazembe kwenye mchezo wao wa mwisho wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Young Africans itakua mgeni wa TP Mazembe Aprili 2 mjini Lubumbashi-DR Congo, katika mchezo wa mwisho, ikumbukwe katika mchezo wao wa kwanza uliopigwa Dar es salaam, Young Africans walishinda mabao 3-1.

Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema kuwa, wanatambua ugumu wa mchezo huo lakini na ndio maana wameamua kutoa nafasi kwa mashabiki kwenda Lubumbashi kwa ajili ya kuwapa nguvu Wachezaji watakapokua katika majukumu ya kusaka alama muhimu zitakazowawezesha kuongoza msimamo wa Kundi D.

“Tuna mchezo dhidi ya TP Mazembe tunakumbuka tulipocheza nao hapa tulishinda na sasa tunawafuata tukiwa na ari ileile ya kusaka ushindi na kupata pointi tatu muhimu.”

“Mashabiki tunatambua umuhimu wao na kuja kwao kutaongeza nguvu ndio maana tumejiandaa kuhakikisha tunabeba alama tatu.” Amesema kamwe

Kikosi cha Young Africans kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam leo Alhamis (Machi 30) kuelekea mjini Lubumbashi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania ‘Air Tanzania’.

Msafara wa Klabu hiyo kuelekea Kubumbashi utakaokuwa na jumla ya watu 44 pia atakuwemo mfadhili Ghalib Said Mohamed (GSM) na Rais wa Young Africans injinia Hersi Said.

Chamberlain ajiweka njia panda England
Ruvu Shooting kumaliza Ligi Kuu kibingwa