Utani ukizidi ni shida, kwani Yanga ilipanga kuondoka leo saa 1:00 asubuhi kwenda Zanzibar, lakini imelazimika kufuta safari yake baada ya kubaini wangepanda boti moja na Simba katika safari yao.

Timu zote hizo zinakwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo imeanza jana Ijumaa usiku kwa kushirikisha timu za Zanzibar, Tanzania Bara na Uganda.

Mchezo ulikuwa hivi, Yanga ilikatiwa tiketi ya boti ya Kilimanjaro kwenda Zanzibar leo saa 1:00 asubuhi, walipododosa wakabaini katika boti hiyo pia kikosi cha Simba kitakuwemo.

Kuona hivyo, viongozi wa Yanga wakalazimika kubadili tiketi za timu yao na kusogeza muda hadi saa 9:00 alasiri watakapoanza safari lengo likiwa ni kutopanda boti moja na Simba.

Mmoja wa viongozi wa Yanga, alilithibitishia Championi Jumamosi kuhusu hali hiyo na kusema sasa kila kitu kipo sawa na wao watapanda boti yao alasiri na siyo ile ya asubuhi na Simba.

“Hivi itawezekana vipi mtu usafiri na adui wako? Kwetu hakuna kitu kama hicho wao kama Simba wanaona sawa kusafiri na sisi kwenye boti sawa, lakini sisi kwetu hapana hatuwezi,” alisema bosi huyo.

Alipotafutwa Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh kuzungumzia sakata hilo alisema: “Ni kweli tulipanga tuondoke kesho (leo) saa moja asubuhi na boti la Kilimanjaro, lakini tumebadili muda na tutaondoka saa tisa alasiri.”

Kwa upande wa Simba, Mussa Mgosi alisema: “Sisi tunaondoka kesho (leo) asubuhi na tutaondoka na kikosi chote tulichokisajili na nisingependa kuwazungumzia wapinzani wetu.”

chanzo: Championi

Cheka Awajibu TPBC, Asema Adhabu Inawahusu Wenyewe
Aunty Ezekiel: ikitokea kwenye muvi natakiwa kukiss najifikiria sana