Uongozi wa klabu bingwa Tanzania bara Young Africans umetilia mkazo rufaa yake dhidi ya African Lyon kumchezesha mchezaji wa Mbao FC, Venence Ludovick.

Katibu wa Young Africans, Baraka Deusdedit ameiambia Dar24 kwamba kanuni zipo wazi, timu inapomchezesha mchezaji ambaye si halali inapaswa kupokonywa pointi.

“Hatushitushwi na propaganda zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba eti Lyon haina makosa kumtumia mchezaji huyo kwa sababu walipewa leseni na TFF, sisi tunatazama kanuni zinasemaje” Alisema Deusdedit.

Aidha, Katibu huyo wa Young Africans alisema kwamba wanalifuatilia kwa makini suala hilo ili kuhakikisha haki inatendeka.

Young Africans imeikatia rufaa African Lyon kwa kumtumia mchezaji Venence Ludovick Desemba 23, mwaka jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja kwa madai ni mali ya Mbao FC ya Mwanza.

Mbao FC pia imekata rufaa na kuiwekea pingamizi Lyon kumtumia mchezaji hiyo.

Ludovick aliichezea Mbao FC mzunguko wa kwanza, kabla ya mzunguko wa pili kuhamia Lyon na akaifunga bao la kusawazisha timu hiyo wakati wa mchezo dhidi ya Young Africans.

Tayari Shirikisho la Soka nchini (TFF), limesema suala la mchezaji huyo linaendelea kufanyiwa kazi na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji.

“Tunawahakikishia umma wa wapenda soka nchini kuwa haki itatendeka kwa mujibu wa kanuni zinazoendesha mashindano husika,”ilisema taarifa ya TFF iliyotumwa katika vyombo vya habari.

Batshuayi Kurudi Ufaransa
JPM: Kila mtu atabeba msalaba wake