Rais wa Rwanda, Paul Kagame anatarajia kuafanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Aprili 27-28, 2023 akiongozana na ujumbe wake unaotarajia kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Aprili 27, 2023 na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax.
Akiwa nchini, Rais Kagame atakutana na kufanya mazungumzo na Mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ikulu Jijini Dar es Salaam, ambapo Viongozi hao Wakuu wataongea na Waandishi wa Habari, kuelezea yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo yao.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliodumu kwa muda mrefu ambapo nchi hizi mbili zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo biashara na uwekezaji, nishati, uchukuzi, elimu na utamaduni.
Kufanyika kwa ziara hii, ni ishara nzuri ya kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa kidugu baina ya mataifa haya kwa maslahi mapana ya pande mbili.