Serikali ya Zimbabwe imefunga mitandao ya kijamii inayotumika zaidi nchini humo wakati ikijaribu kuzima maandamano makubwa yaliyozuka kupinga kupanda kwa gharama za bidhaa na ukosefu wa ajira.
Mitandao iliyofungwa ni pamoja na Facebook, Twitter na WhatsApp ambayo ilibainika kutumika zaidi kuwaunganisha wananchi na kuwahamasisha kushiriki maandamano hayo.
Muungano wa taasisi za kutetea haki za binadamu nchini humo umeeleza kuwa hadi sasa watu 12 wamepoteza maisha kutokana na maandamano hayo na kwamba kuna idadi kubwa ya majeruhi pamoja na baadhi ya wanaoteswa na vyombo vya usalama kwa kushukiwa kuwa viongozi wa makundi ya maandanao.
Jukwaa la Haki za Binadamu la Zimbabwe ambalo ni moja kati ya taasisi zisizo za kiserikali, limelaani kitendo hicho cha kuzimwa kwa mitandao kwa madai kuwa kinalengo la kuzima sauti ya wananchi.
Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa Serikali ya Zimbabwe kutotumia nguvu kupita kiasi.
“Chama cha Madaktari [Zimbabwe] kimesema kuwa zaidi ya watu 60 wametibiwa hospitalini kutokana na majeraha ya risasi, hii sio njia sahihi ya kuzima maandamano yanayopinga hali ya uchumi,” Reuters inamkariri Msemaji wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Ravina Shamdasani.
Alhamisi, mwanaharakati maarufu, Enan Mawarire aliyehamasisha mgomo wa watu kutokwenda makazini kwa siku tatu kupitia mtandao wa kijamii, alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kuhujumu Serikali. Endapo atakutwa na hatia anaweza kufungwa hadi miaka 20 jela kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo.
Rais Emmerson Mnangagwa amewataka wananchi kutulia wakati Serikali yake inafanya jitihada za kuimarisha uchumi, ikiwa ni pamoja na kuomba msaada kwa washiriki wao na kuwaalika wawekezaji zaidi.
Wiki hii, Rais Mnangagwa alikuwa nchini Urusi ambapo alikutana na Rais Vladimir Putin na kumuomba kusaidia kuimarisha uchumi wa nchi hiyo.