Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema kuwa hali ya chakula nchini siyo nzuri kutokana na uhifadhi mbaya wakati  Serikali ikisema hali ni shwari licha ya baadhi ya maeneo kutopata mvua za wastani.

Zitto amesema Ghala la Taifa la Chakula (SGR) lina hifadhi ya chakula kinachotosha kwa siku nane tu wakati Novemba 2015 kulikuwa na chakula cha kutosha miezi miwili.

“Hali ya chakula inazidi kuwa mbaya kwa sababu ya maamuzi mabovu ya Serikali kuhusu hifadhi ya chakula. Serikali zote zilizopita huko nyuma zilikuwa zinanunua chakula cha akiba ili wakati wa ukame kama sasa chakula hicho kiingie sokoni, hivyo kushusha bei na kuwezesha wananchi kumudu gharama za chakula,”amesema Zitto.

Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba amejibu madai hayo ya Zitto akisema nchi ina chakula cha kutosha wala siyo cha siku nane wala mwezi pekee, bali zaidi.

“Kuna maeneo mahindi yameanza kukomaa na wakulima wa huko watavuna kama kawaida, tunachokifanya tutadhibiti uuzaji wa chakula nje ya nchi bila vibali ili chakula kisambae zaidi kwa Watanzania. Japo siwezi kutaja kiasi cha chakula kilichopo kwa sababu za kiusalama, ila kinatosha siyo kwa siku nane wala mwezi mmoja bali ni zaidi,” amesema Tizeba.

Kinachojili kuhusu vitabu vya darasa la kwanza vyenye makosa chaanikwa
Mwigulu awaonya wakulima na wafugaji kilosa