Mtayarishaji wa muziki wa Bongo Fleva, Abidad na msanii wake Modala wamemuomba radhi Ommy Dimpoz kwa kumshambulia kwa tuhuma za kuiba wimbo wao ‘Cheche’ ambao wote wanadai walipewa na mwandishi wa mashairi na melodi, Lollipop.

Akifunguka kupitia E-News ya East Africa TV, Abidad amesema kuwa anamuomba radhi Ommy Dimpoz kwa kitendo cha kumuandikia ujumbe kwenye post yake ya Instagram akimtuhumu kwa kuiba wimbo huo, lakini sasa amebaini kuwa msanii huyo hana hatia.

“Ningeomba nimuombe samahani [Ommy Dimpoz] kwa sababu nilienda ku-comment kitu pale, kwamba yeye ndiye aliyehusika kufanya hicho kitendo,” alisema Abidad.

“Ilikuwa ni hasira kwanza. Na baada ya kucomment sikuweza kumtafuta Ommy direct (moja kwa moja), lakini ilikuwa ni hasira tu. Kwa sababu Ommy Dimpoz yeye hana kosa,” aliongeza.

Mtayarishaji huyo wa muziki alikiri pia kuwa hajamtafuta Lollipop hadi sasa kuzungumzia suala hilo kwani anaamini alifanya kitendo cha dharau kuandika wimbo na kuwapa wote wawili kwa nyakati tofauti.

“Niliona ni kitendo cha dharau kwangu. Sikuwa na tofauti na Lollipop kabla, na ndio maana na mimi nikashangaa kwanini lilifanyika hili,” Abidad alifunguka.

Katika hatua nyingine, Modala ambaye ndiye msanii aliyeimba ‘Cheche’ awali anayodai alipewa na Lollipop pia alimuomba radhi msanii huyo ambaye ni mwanafamilia mpya wa Rockstar4000 akieleza kuwa amebaini hana hatia bali lawama zote zimuendee Lollipop ambaye amedai hakuwa mwaminifu.

“Kama kuna kitu ambacho mimi nilimkwaza Ommy Dimpoz naomba anisamehe, na sidhani kama nilimuongelea vibaya na bahati nzuri siku-comment kwenye ukurasa wake mimi binafsi,” alisema Modala.

Alisema ameamua kuachana na wimbo huo kwa sababu Ommy Dimpoz tayari ameshausajili wimbo lakini wao hawajasajili.

Kwa upande wa timu ya Lollipop, mtayarishaji wa muziki, Kidbwoy ambaye ni mwanafamilia wa ‘Dope Tunes’ ambao ndio waliomuuzia wimbo Ommy Dimpoz na kuuandaa, amesema kuwa ameshangazwa na tuhuma za Abidad kwa Lollipop kupitia vyombo vya habari hata bila kumtafuta mhusika kwanza.

Kidbwoy aliongeza kuwa Lollipop ambaye ni msanii wa nyimbo za injili akitambulika kama Goodluck Gozbert hajajitokeza kwenye vyombo vya habari kwakuwa yuko bize akiandaa mradi wake mpya wa nyimbo za injili.
Usikilize ‘Cheche’ hapa:

Trump ajitathmini, aanza kulegeza misimamo yake
Kinda La Chelsea Lang'oka Jumla Stamford Bridge