Kocha wa klabu ya Simba, Patrick Aussems amesema kuwa anaamini klabu yake inaweza kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida United, uliopigwa jana Jumamosi.

Amesema kuwa kundi la Simba katika Klabu Bingwa liko wazi na yeyote anaweza kupata nafasi ya kufuzu lakini akiamini timu yake inayo nafasi kubwa kutokana na sapoti kubwa ya mashabiki hasa katika michezo ya nyumbani.

“Nafikiri ni kundi ambalo liko wazi, hata kama tuko na timu mbili ambazo zilicheza fainali msimu uliopita. timu hizi zimecheza mechi ngumu sana katika siku za karibuni na hazitakuwa na muda wa kupoteza,” amesema Aussems.

Simba imepangwa kundi D pamoja na Al Ahly ya Misri, AS Vita ya Congo DRC na JS Saoura ya Algeria.

Al Ahly ilicheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Esperance Tunis ya Tunisia ambapo Esperance ilishinda ubingwa kwa uwiano wa mabao 4-3 huku AS Vita Club ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.

Hasunga aagiza wakulima wasajiliwe
Chadema yagonga mwamba kwa Mbowe, yapigwa marufuku

Comments

comments