Leo Desemba 30, 2016 Kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBC) imetangaza kumfungia kwa miaka miwili Bondia wa ngumi za kulipwa, Francis Cheka kufuatia kitendo chake cha kugoma kupanda ulingoni kupigana na Bondia Abdallah Pazi “Dullah Mbabe”.

TPBC wamesema kitendo hicho kilichofanywa na Cheka kinaashiria uwezekano mkubwa wa kupoteza uaminifu baina ya mabondia na waandaaji wa mapambano, kujiondoa kwa waandaaji katika mchezo huo kwa kuona hakuna uaminifu na pia kinaweza sababisha uvunjifu wa amani kwa watazamaji, iwapo wataendelea kudanganywa uwepo wa mapambano hewa.

Pambano hilo ilikuwa lifanyike Desemba 25 mwaka huu, katika Ukumbi wa PTA Saba saba jijini Dar es salaam, lililoandaliwa na Promota Siraju Kaike kupitia kampuni yake ya Kaike Promotion.

Katibu Msaidizi wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBC), Chatta Michael ameviambia vyombo vya habari kuwa Kamisheni yake ilitoa kibali cha kufanyika kwa mpambano huo baada ya kujiridhisha kuwa taratibu zote zimefuatwa na mabondia wameridhia na kukubaliana na muandaaji, Ila wameshangwaza na Bondia Francis Cheka kugoma kupanda ulingoni kwa madai ya malipo wakati alishasaini mkataba na muandaaji ulioonyesha kuwa ameshachukua kiasi cha shilingi milioni tatu (3,000,000) na baada ya mpambano alitakiwa kupewa kitita chake cha milioni sita.

Hivyo Kamati ya utendaji ya Kamisheni hiyo iliyokaa Desemba 27, na kupitia kanuni za mchezo huo, imemkuta Bondia Francis Cheka na makosa ya kimakubaliano na kutangaza kumfungia kujihusisha kwa namna yeyote na mchezo huo na kutakiwa kulipa faini ya shilingi laki tano (500,000).

Video: Meya wa kinondoni azindua mradi wa uboreshaji jiji la Dar es salaam
Young Africans, Simba SC Kuelekea Unguja Kesho