Washika bunduki wa kaskazini mwa jijini London (Arsenal) wana matarajio makubwa ya kumsajili kiungo kutoka nchini Uswiz na klabu ya Borussia Monchengladbach ya Ujerumani, Granit Xhaka.

Arsenal wanajipa matumaini hayo, kutokana na kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao, na wanaamini kiu kubwa na Xhaka ni kuonekana akiwa sehemu ya kikosi kitakachoshiriki michuano hiyo.

Gazeti la Daily Mirror la hii leo, limechapisha habari inayosema kwamba, Arsenal wametenga kiasi cha paund million 33.8, kwa ajili ya kukamilisha mpango wa kumnasa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23.

Wakati Arsenal wakijiandaa na ofa hiyo, mkurugenzi wa michezo wa klabu ya Borussia Monchengladbach, Max Eberl amethibitisha uwezekano wa Xhaka kuondoka wakati wa majira ya kiangazi, lakini akaonyesha walakini kutokana na ofa ya usajili wake kutokuwafikia hadi sasa.

Amesema lolote linaweza kutokea katika kipindi hiki, na wao kama viongozi hawana hiyana ya kumzuia Xhaka kuondoka kama watapokea ofa nzuri ambayo itakuwa na manufaa na klabu ya Borussia Monchengladbach.

“Msimu umeshamalizika, na unapozungumzia usajili ni jambo la kawaida hivyo tunatarajia mambo mengi kutoka katika klabu kadhaa za hapa Ujerumani pamoja na kwingineko kuhusu wachezaji wetu,” amesema Max.

“Maamuzi ya kuuzwa kwa Xhaka pamoja na wachezaji wengine watakaotakiwa na klabu zitakazoonyesha nia, yatafanywa na uongozi kwa ujumla, hivyo tusubiri na kuona kama hilo litatokea,”

“Mimi sio mtu sahihi wa kukupa majibu kama Xhaka ama wachezaji wengiene watauzwa ama la, lakini ninachofahamu ofa za klabu kadhaa huenda zikaanza kuwasili wakati wowote kuanzia sasa.” Aliongeza Max Eberl alipokua akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti la Daily Mirror.

Callum Wilson, Matt Ritchie Wawanyima Usingizi West Ham Utd
Zlatan Ibrahimovic Awapa Masharti Man Utd