Kiungo mpya wa klabu Bingwa Tanzania Bara Wekundu Wa Msimbazi Simba, Larry Bwalya amesema amefurahi kujiunga na miamba hiyo ambayo sasa itamkutanisha katika klabu moja na Clatous Chama kama ilivyo kwenye timu ya Taifa ya Zambia.

Bwalya ambaye amejiunga na Simba katika dirisha hili la usajili akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia, timu ya zamani ya Chama, amesema amefurahi kumkuta kiungo mshambuliaji huyo ndani ya Simba na anaamini watacheza vizuri na kuisaidia timu hiyo kupata mafanikio wakishirikiana na nyota wengine.

Wawili hao wanaichezea Chipolopolo, jambo ambalo linamfanya Bwalya kueleza kuwa  watatengeneza maelewano makubwa wakishirikiana na wachezaji wengine ndani ya kikosi cha Simba.

Bwalya ambaye anaweza kucheza nafasi zote za safu ya kiungo wa ulinzi na ushambuliaji kwa ufasaha, alisema jijini juzi kuwa baada ya kupokea ofa ya klabu hiyo hakufikiria mara mbili kuikubali kwa kuwa Simba ni timu yenye historia kubwa na amependa kuwa sehemu ya historia hiyo.

“Nimefurahi kucheza pamoja na Chama kwenye timu moja kama ilivyo timu ya Taifa. Ninaamini kwa pamoja tutafanya vizuri pamoja na wachezaji wengine kwa ajili ya kuisaidia timu kupata ushindi.

“Simba ni klabu yenye historia kubwa na ninapenda kuwa sehemu ya historia hiyo, kikubwa tunaomba mashabiki waendelee kutusapoti tunaamini tutafanya vizuri,” alisema Bwalya akizungumza na tovuti ya klabu hiyo.

Mashabiki wa Simba wataanza kumshuhudia Bwalya Uwanja wa Mkapa Jumamosi pamoja na nyota wengine waliosajiliwa msimu huu watakaposhuka dimbani katika Tamasha la Simba Day kuivaa Vital’O ya Burundi.

Mbali na Bwalya, wachezaji wengine wapya watakaotambulishwa Jumamosi ni Ibrahim Ally Ame kutoka Coastal Union, Charles Ilamfya (KMC), David Kameta (Lipuli FC), Chriss Mugalu (Lusaka Dynamos), Joash Onyango (huru) aliyemaliza mkataba na Gor Mahia ya Kenya na Benard Morrison (huru) baada ya kumaliza mkataba na Yanga.

Baada ya mechi hiyo, kituo kitakachofuata kwa Simba kitakuwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha tayari kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo FC utakaopigwa Agosti 30.

Mchezo huo utakuwa maalum kwa ajili ya kukaribisha msimu mpya wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza Septemba 6, mwaka huu, huku mabingwa watetezi hao wakifungua dhidi ya Ihefu FC mechi ambayo itapigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mali: viongozi wa mapinduzi wazungumza na upinzani
Wa Nec 54 kikaangoni leo