Klabu ya Chelsea ipo katika mazungumzo na uongozi wa klabu ya Athletic Bilbao, kwa ajili ya kufanikisha usajili wa mlinda mlango kutoka nchini Hispania Kepa Arrizabalaga Revuelta.

Chelsea wamevutiwa na uwezo wa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 23, na wanaamini ataweza kuziba nafasi ya Thibaut Courtois, ambaye yu njiani kujiunga na mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa, huenda mlinda mlango huyo ukawagharimu Chelsea kiasi cha Pauni milioni 71.6.

Akizungumza mara baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Olympic lyon usiku wa kuamkia leo, meneja wa Chelsea Maurizio Sarri alisema: “Niliwahi kumuona mwaka mmoja uliopita.

“Nilivutiwa na kiwango chake, ana uwezo wa kuhimili mikiki mikiki ya timu pinzani anapokua langoni, licha ya kuwa na umri mdogo.”

Taarifa kutoka Hispania zinaeleza kuwa, mpaka jana Jumanne, pande hizo mbili zilikua zinaendelea na mazungumzo ya kuangalia uwezekano wa kufanya biashara ya mlinda mlango huyo, ambaye huenda akawa ghali zaidi duniani, endapo atasajiliwa kwa kiasi kilichotajwa.

Chelsea pia wanahusishwa na taarifa za kuwasajili walinda mlango Diego Rico na Jack Butland, lakini Kepa anaonekana kupewa kipaumbele zaidi kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili kesho Alkhamis.

Butland anaendelea kuwa katika orodha ya wanaofikiriwa huko Stamford Bridge, kutokana na thamani yake kuwa ndogo, tofauti na walinda mlango wengine.

Mlinda mlango huyo kutoka nchini England, thamani yake ni Pauni milioni 30.

Wakati huo huo uongozi wa klabu ya Real Madrid unajipanga kumtoa kwa mkopo kiungo Matteo Kovacic kwenda Chelsea pamoja na kiasi cha fedha, ili kukamilisha usajili wa mlinda mlango Courtois.

DC Joketi: Sheria itachukua mkondo wake kwa atakaye kaidi agizo
Video: Inauma sana kumteua mpinzani- Msukuma

Comments

comments